Header Ads Widget

WAKAZI WANAOTAKIWA KUPISHA ENEO LA JESHI KISARAWE WAMWANGUKIA RAIS SAMIA

Mzee Geofrey Mdoe akionyesha kwa waandishi (hawapo) pichani paa la duka lake lilivyochakaa.

Wakazi wa Bomani wakiwa pamoja kujadiliana kuhusu hatima ya malipo yao ya fidia kupisha eneo la jeshi
Mmoja wa wananchi hao akionyesha uchakavu wa kilichokuwa choo chake.

xxxxxxxxxx

NA MWANDISHI WETU, MATUKIODAIMA App

Wakazi wa eneo la Bomani katika Mji mdogo wa Kisarawe wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuwasaidia kulipwa fedha za fidia ya makazi yao kwa ajili ya kupisha eneo la Jeshi Kikosi cha 191 wilayani humo mkoani Pwani.


Wakazi hao 31 wa eneo la Bomani maarufu ‘barabara ya jeshi’, waliwaambia waandishi wa habari juzi Februari 21 mwaka huu kuwa, kwa pamoja wamekubali kuhama kupisha eneo hilo kama walivyotakiwa na mamlaka za Serikali.


Akizungumza kwa niaba ya wenzake, kiongozi wa wananchi hao, Robert Nyampiga alisema waliuziwa nyumba hizo zilizopo hatua chache kutoka ilipo Kambi ya Jeshi Kikosi cha 191 na Serikali kupitia Wakala wa Nyumba mwaka 2005.


Alisema tathmini ya nyumba na makazi yao ilikwishafanyika na wamefuatilia hadi hazina lakini hawajapata muafaka wowote wa lini wataingiziwa malipo yao ya fidia ili waondoke kwenye eneo hilo.


“Nyumba hizi wengi tulionunua ni wastaafu kutoka sekta mbalimbali, na baadhi yetu tulikwishafungua biashara ndogo ndogo ili kupata mahitaji ya kujikimu, lakini walipotutaka kuhama pia walitwambia tusiendeleze kitu chochote labda tulime mchicha tu kwani tungelipwa ndani ya miezi minne.


“Hata hivyo, mpaka sasa yapata mwaka sasa hatuoni chochote, hatuambiwi chochote tumebaki na sintofahamu” alisema Nyampiga.


Mzee Geofrey Mdoe ambaye pia ni miongoni mwa wananchi hao, alisema hali imekuwa ngumu sana kwao baada ya nyumba zao kuanza kuvuja na kuharibika kabisa.


“Tunazidi kuwa na wasiwasi kwamba hili eneo bado linatakiwa na wahusika, tunashangaa tangu tumefanyiwa tathmnini yapata mwaka mmoja sasa, sasa kama hili eneo hawalitaki tena wafute tathmini yao ya awali ili sisi tuendelee kufanya maendeleo katika nyumba zetu.


“Ndugu mwandishi angalia hili ni duka langu (anamwonyesha mwandishi paa la duka lake), nimelifunga kwa sababu linavuja lote na siwezi kubadilisha hata bati, kimsingi tumefungwa mikono na miguu, tunahitaji kauli na vitendo kutoka kwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan.”alisisitiza Mzee Mdoe.


Mhanga mwingine, Maliselina Macha alisema kinachomuumiza alifunga biashara zake baada ya kuambiwa wanatakiwa kuhama ndani ya miezi minne. Alisema alikuwa na duka la vinywaji ambavyo alivinunua kupitia mkopo wa halmashauri na kulazimika kuviuza kwa hasara akitarajia kuhama katika eneo hilo.


“Niliamua kuuza bidhaa zote za dukani pamoja na mifugo yangu ili kupisha makazi haya ambayo tuliambiwa nikwa ajili ya usalama. Hatuna pingamizi na hilo isipokuwa jambo hili limetusababishia msongo wa mawazo, nyumba zetu zimebomoka, hatuna mahali hata pa kujisaidia, tunateseka hatima yetu hatuijui, tumaini letu pekee ni kwa mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan kupitia taarifa hizi atuone na kutusaidia” alisema Maliselina.


MATUKIODAIMA lilimtafuta Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Fatuma Almasi Nyangasa ili kuzungumzia suala hilo lakini hakupatikana. Juzi Februari 21,2024 Katibu mukhtasi wake alisema mkuu huyo alikuwa kikaoni.


Hata alipopelekewa ujumbe wa maandishi na hata wa simu ya mkononi hakujibu.


Kwa upande wake, Kamishna wa majengo na maeneo yote ya jeshi, Kanali Yenu Maguguli alipoulizwa alisema wenye mamlaka ya kufanya malipo hayo ni hazina, hivyo aliwataka wananchi hao kuvuta subira kwani anaamini haki itatendeka.

Post a Comment

0 CommentsMAGAZETIBBC NEWS