Na Shemsa Mussa,Kagera
TAASISI ya kuzuia na kupambana na Rushwa Mkoa wa Kagera imefuatilia na kuokoa miradi 19 yenye zaidi ya shilingi bilioni 6.1 ambapo kati ya hiyo miradi 16 yenye zaidi ya shilingi bil.4.2 imebainika kuwa na mapungufu na kiasi hicho ni sawa na asilimia 68.50 ya fedha za miradi ambapo kumekuwa na ongezeko la asilimia 18.77 ya miradi hiyo, ukilinganisha na kipindi cha Julai-Septemba mwaka jana.
Ameeleza hayo leo Kamanda wa Takukuru Mkoani humo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu yao kwa kipindi cha robo tatu ya mwisho wa mwaka 2023 ambapo,miradi iliyohusika ni ya ujenzi wa Miundombinu ya shule mpya za msingi na Sekondari,Maji,zahanati pamoja na ujenzi wa madarasa ya msingi na sekondari ili kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kuendana na thamani ya fedha iliyotumika.
Mwakasege amesema kuwa kwa kipindi hicho walipokea malalamiko 92 kati ya hayo 58 hayahusu rushwa ambapo 34 yanahusu rushwa na majalada yamefunguliwa ambapo 20 uchunguzi wake umekamilika na hatua stahiki zinatarajiwa kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria.
“Idara zilizoonekana kuwa na dosari ni Halmashauri ambapo idara ya fedha kesi moja,Elimu 10,Afya saba,utawala 12,Biashara moja,kilimo 8,Ardhi 7,mazingira 3 na mengine yalihusu sekta binafsi ambayo ni 12,maji 3,ujenzi 9,maliasili 7,Nishati 1,Uhamiaji 2,polisi 4,mahakama 3,uchukuzi 1 na mamlaka ya mapato Tanzania (TRA )moja "amesema Mwakasege.
Amesema katika progaramu ya Takukuru rafiki ambayo inatekelezwa kwa kushirikisha wadau katika ngazi ya kata ambapo wananchi hupata fursa ya kuibua kero zinazowakabili katika maeneo yao ambapo kwa kipindi cha Oktoba-Desemba walitembelea kata 11 na kupokea kero kuhusu sekta za Elimu,Afya,maji,fedha na Nishati ambapo ufuatiliaji wake unaendelea.
Aidha amevitaja vipaumbele vya Takukuru kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Machi mwaka huu ambavyo ni kuelimisha Umma kupitia njia mbalimbali ili kuongeza ushirikishwaji wa wananchi katika kuzuia vitendo vya rushwa,kutatua kero mbalimbali katika jamii kupitia programu ya Takukuru Rafiki na kuendelea kufuatilia rasilimali za Umma kupitia ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ili kuzuia ufujaji wa fedha za Umma.
Nyingine ni kufanya chambuzi za mifumo kwa lengo la kuzuia rushwa zinazosababishwa na mapungufu yaliyopo kwenye mifumo ya utendaji wa sekta ya Umma na sekta binafsi ambapo amewahimiza wasimamizi wa miradi ya maendeleo kuwa waadilifu na kuhakikisha fedha zote za miradi zinatumika vizuri.
0 Comments