Na Thobias Mwanakatwe, DODOMA
LICHA ya serikali kuvifunga viwanda viwili vya kuchinja nyama ya Punda katika mikoa ya Shinyanga na Dodoma lakini biashara ya mnyama huyo inadaiwa kuendelea kufanyika kinyemela.
Hali hiyo inatishia kutoweka kabisa kwa punda hapa nchini kama hatua za makusudi hazitachukuliwa kudhibiti biashara hiyo.
Hayo yamebainika juzi wakati wa mafunzo ya siku mbili ya waandishi wa habari kutoka mikoa ya Dodoma,Singida,Iringa na Shinyanga yaliyoandaliwa na Shirika Lisilo la Kiserika la Inades Formation Tanzania (IFTz) linalojishughulisha na maendeleo ya wakulima,kiuchumi na ustawi wa kijamii.
Mkuu wa Programu kutoka shirika hilo, Jacqueline Nicodemus, alisema pamoja na serikali kuvifunga viwanda vya nyama ya punda na kupiga marufuku biashara ya nyama,ngozi na uchinjaji wa punda lakini bado inaonekana biashara hiyo inaendelea kufanyika kinyemela.
"Pamoja na zuio la serikali lakini bado kuna 'movement' za punda kuelekea maeneo ya Mkoa wa Shinyanga ambapo Februari mwaka huu serikali ilitoa tamko tena kwamba kama kuna mtu yeyote ana mazao ya punda asalimishe wizarani na tangazo hilo limetokana na kuendelea kuwepo kwa 'movement' katika uchinjaji wa punda," alisema.
Nicodemus alisema Shirika la Inades Formation Tanzania (IFTz) kwa kushirikiana na serikali na wadau wengine bado linaendelea kukabiliana na kutoweka kwa punda kwasababu katika jamii inaaminika kuwa ili jamii ziweze kustawi hususani maneo ya vijijini zinahitaji mnyama kazi punda.
Alisema 2021 baada ya kufungwa kwa viwanda vya kuchinja nyama ya punda ambavyo ni Fang Hua kilichokuwa kijiji cha Ibadakuki Manispaa ya Shinyanga na kiwanda Huwa Cheng kilichokuwa Dodoma, kulifanyika mkutano mkubwa jijini Dar es Salaam na kuja na maazimio ya kulinda punda aweze kuendelea kuwepo.
"Katika mkutano huo ilitolewa tamko ambalo liliweka msisitizo wa zuio la serikali ya Tanzania kwamba hakutakuwa na biashara ya zao la punda hadi punda watakapifikia milioni 10 Tanzania," alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Inades Formation Tanzania (IFTz), Mbarwa Kivuyo,alisema shirika hilo limeanzisha kampeni ya kulinda punda na kuhakikisha wanapata haki za msingi za mnyama kwani kwa Sensa iliyofanyika punda waliopo nchini ni 60o,000 tu.
Alisema pamoja na kuwepo kwa sera na sheria na kufungwa kwa viwanda vya kuchinja nyama ya punda lakini bado wanaendelea kuchinjwa sasa lazima tuwe na mkakati wa kumlinda mnyama huyu asitoweke.
"Kuongezeka kwao punda ni kidogo sana wanabeba mimba zaidi ya mwaka na pia kuanzia kubeba mimba na mtoto mwingine kuja kufuata inachukua muda mrefu sasa, tuweke mkazo kumlinda kwani katika suala la uchumi ukimuondoa ng'ombe ambaye yupo juu anayefuata katika 'economic benefits' kwa jamii zetu hususani wafugaji ni punda," alisema.
Washiriki wa mafunzo hayo walisema kuja haja kwa serikali kuangalia namna ya kuwafanya punda wazaliane mara kwa mara kama ilivyo kwa wanyama wengine ili kuongeza idadi.
Kiwanda cha kuchinja nyama ya punda cha Fang Hua kilichokuwa Manispaa ya Shinyanga kilisitishwa kufanya kazi Oktoba 2021 baada ya kukiuka masharti kadhaa ikiwamo kuchinja punda 150 kwa siku badala ya 20 kama makubaliano yalivyokuwa yametolewa.
Nacho kiwanda cha nyama ya punda cha Huwa Cheng kilichokuwa jijini Dodoma kilifunga uzalishaji 2020 kutokana na kukiuka masharti,viwanda vyote hivyo vilikuwa vinamilikiwa na wawezaji kutoka China. Mikoa inayofuga punda kwa wingi hapa nchini ni Shinyanga,Singida na Dodoma.
MWISHO
0 Comments