Header Ads Widget

SEKTA YA ELIMU YAPEWA KONGOLE KUSITISHA MATUMIZI YA KUNI MKAA





Na Hamida Ramadhan Matukio Daima App Dodoma

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Seleman Jaffo amesema Taasisi zote zinazolisha watu zaidi ya 100 kwa siku, kupitia Wizara zenye dhamana na Taasisi hizo, zimetoa taarifa za utekelezaji wa agizo  la kusitisha matumizi ya kuni na mkaa ifikapo Januari 2024.


Dkt Jaffo amesema hayo jijini hapa leo,Februari 20,2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua za utekelezaji wa katazo la matumizi ya kuni na mkaa ambapo amesema lengo la maelekezo ya Rais Samia  ni Kupunguza madhara ya kiafya na Mazingira yanayosababisha na kukithiri kwa matumizi ya kuni na mkaa katika jamii.


Amesema katika Sekta ya Elimu,

utekelezaji wa agizo la Serikali umefanyika ambapo hadi kufikia tarehe 31 Januari 2024, jumla ya Vyuo vya Ualimu 30 kati ya 35 sawa na asilimia 85.71 ya lengo, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 51 kati ya 54 sawa na asilimia 94.44 ya lengo, na Vyuo vya Elimu ya Ufundi (VETA) vinane (8) kati ya 36 sawa na asilimia 22.22 vimeshaunganishwa na huduma ya Nishati mbadala ya Kuni Poa (Clean Energy Briquettes) na Gesi.


 "Serikali inaipongeza Wizara ya Elimu kwa kuwa kinara kwa taasisi zake nyingi kutekeleza agizo hilo la serikali kwa zaidi ya asilimia 85," Amesema Waziri Jafo. 


" Na kuongeza taasisi zingine zinapaswa kuiga mfano mzuri uliofanywa na Wizara ya Elimu na Taasisi zake, ''amesema


Hata hivyo ameeleza kuwa takwimu za uharibifu wa misitu nchini zinaonesha kuwa takriban hekta 469,420 za misitu zinapotea kila mwaka kutokana na matumizi yasio endelevu ya rasilimali za misitu ikiwemo uvunaji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.


"Hali hiyo imekuwa ikisababisha madhara makubwa ikiwemo kupungua kwa vyanzo vya maji, kuwepo kwa vipindi virefu vya ukame na kupotea kwa bioanuai,"amesema.


Na kuongeza "Ofisi yake ipo katika maandalizi ya kuunda timu ya wataalamu itakayoweza kutembelea taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kwa siku ikiwa ni kutekeleza agizo la Dkt.Rais Samia Suluhu Hassan


Amesema mtakumbuka kuwa katika kutekeleza maelekezo ya Rais, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais ilitoa katazo la matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi zinazoandaa na kulisha watu zaidi ya mia moja (100) kwa siku, ifikapo Januari, 2024.


Ameeleza kuwa Taasisi hizo ziko chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Afya, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. 


Amebainisha kuwa Taasisi hizo zilielekezwa kuwasilisha mipango yao ya kuhama kutoka matumizi ya kuni na mkaa na kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.


"Wizara zote zimetuma mipango husika ya matumizi ya nishati mbadala na jinsi zitakavyotekeleza agizo hilo na Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa kanzidata ya taarifa kutoka Wizara zinazotekeleza katazo hilo ili kuweza kufuatilia utekelezaji wa agizo hilo,"amesema.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI