NA WILLIUM PAUL, Mwanga.
VIJANA wametakiwa kuepuka kutumika vibaya kisiasa na kugawanywa makundi katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani 2025.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Ivan Moshi wakati akizungumza na vijana katika maadhimisho ya miaka 47 tangu kuzaliwa kwa CCM, yaliyofanyika katika kata ya Kileo, wilaya ya Mwanga,mkoani humo.
Moshi ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya utekelezaji wa UVCCM Taifa, amesema, vijana kama nguvu kazi ya Taifa wanapaswa kuwa imara katika kukipigania chama hicho na kudumisha umoja, mshikamano na upendo katika kipindi hiki na kuepuka chuki na majungu.
“Ndugu zangu vijana, mwaka huu tuna uchaguzi wa serikali za mitaa na mwakani 2025 uchaguzi Mkuu, niwaombe vijana wenzangu, tusikubali kutumiwa vibaya na watu kwa maslahi yao binafsi, tuweke mbele maslahi mapana ya chama na Taifa”
Ameongeza kuwa, “Tunatambua lengo la chama chochote cha siasa ni kushika dola, na kazi hiyo sisi vijana wa UVCCM tuifanye kwa umoja kama chama, tusigombane na tusigombanie nafasi. Ukiona umegombea ukakosa, muunge mkono yule aliyeshinda, na kuimarisha umoja na upendo, tusikubali kugawanywa makundi na kuendekeza chuki na majungu”.
Katika hatua nyingine, Moshi ametoa rai kwa viongozi wa vitongoji, vijiji na hata mitaa, kujenga utamaduni wa kukaa na wananchi kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili katika maeneo yao ili kuziwasilisha katika ngazi husika na kuweza kutafutiwa ufumbuzi.
“Wananchi wanahitaji kusikilizwa na kusemewa matatizo yao, sasa viongozi wetu wa vijiji hata madiwani na wabunge, kaeni na wananchi kujua ni nini kinawakabili, leo wananchi wanalalamika kwa sababu viongozi ikiwemo wale wa kuchaguliwa, hamtoki kuzungumza nao na kupanga nao namna ya utatuzi wa changamoto zao”
Akizungumza Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Moshi vijijini, Yuvenal Shirima amewataka vijana wenye sifa kujitokeza kuchukua fomu na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa na hata uchaguzi mkuu wakati utakapofika, ili nao kuwa sehemu ya maamuzi.
Aisha Mfaume Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Mwanga, amewataka vijana kuwa waadilifu na kuendekea kukipigania chama katika kipindi hiki cha kuekekea uchaguzi ili kuhakikisha kinapata ushindi.
0 Comments