NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MKOA wa Kilimanjaro umepokea jumla ya magari 15 katika Sekta ya Afya kati ya hayo magari 10 ni ya kubebea wagonjwa (Ambulance), na magari 5 ni kwa ajili ya utawala ambayo yatatumika kwenye huduma za usimamizi shirikishi na usabazaji chanjo.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu ambapo alisema kuwa, Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya mapinduzi makubwa na uwekezaji katika miradi ya Maendeleo hususani sekta ya Afya.
Babu alisema kuwa, lengo la kuborsha sekta ya afya ni kuhakikisha Makundi yote kwenye jamii yanapata huduma za afya bora na zenye viwango vinavyotakiwa ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020/2025.
“Magari haya ymepatikana kutokana na jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za afya bora na zenye viwango hivyo magari haya yatumike kwa lengo lililokusudiwa na si vinginevyo” alisema Babu.
Mkuu huyo wa mkoa alisema mgawanyo wa magari ya kubebea wagonjwa ni kama ifuatavyo ambapo halmashauri ya same imepokea magari mawili, halmashauri ya Moshi magari mawili, Manispaa ya Moshi magari mawili, Rombo, Siha, Mwanga, Hai zenyewe zikipata gari moja moja.
Aidha alisema kuwa, mkoa umepokea magari ya utawala matano ambapo Ofisi ya Mkuu wa mkoa gari moja, Halmashauri ya Siha, Hai, Rombo na Moshi zikipata kila moja gari moja.
Alisema kuwa, uwepo wa magari hayo ni ukombozi mkubwa kwa jamii kuweza kupata huduma za afya bora na kwa wakati hasa pale inapohitajika kwenda vituo vya afya vya ngazi ya juu kupata huduma za kibingwa.
Babu alisema kuwa, uwepo wa magari hayo pia utasaidia kuboresha huduma za afya ya uzazi na motto hasa kupitia mfumo wa m-mama ambao lengo lake kubwa ni kutoa huduma ya dharura kwa kina mama wajawazito, mama aliyejifungua na mtoto mchanga.
“Uwepo wa magari haya ya wagonjwa itasaidia sana kuwahisha kina mama na watoto wenye dharura katika vituo vya ngazi ya juu ili waweze kupata huduma stahiki na kwa wakati hii itasaidia sana kupunguza ucheleweshaji wa wagonjwa na hivyo kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi” alisema Babu.
Babu alitoa wito kwa viongozi wa sekta ya afya ngazi zot, Watumishi wa sekta ya afya na jamii kuwa walinzi wa vyombo hivo kwani Serikali imeingia gharama kubwa sana kununua na kuwataka kuvitunza na kuhakikisha usalama wake upo vizuri na kuwataka magari hayo kutumika kama ilivyokusudiwa.
Mwisho...
0 Comments