Header Ads Widget

MIILI YA WATUMISHI WA YWAM ARUSHA WALIOKUFA KWA AJALI YAAGWA

 


NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA



Miili ya watumishi wawili waliofariki katika ajali iliyotokea Februari 24 katika eneo la kibaoni Ngaramtoni katika barabara ya Arusha-Nairobi ambao ni wafanyakazi wa shirika la Youth With A Mision(YWAM) Arusha imeagwa rasmi leo kwa ajili ya kusafirishwa kwaajili ya maziko nchini Kenya pamoja na wilayani Magu  mkoani Mwanza huku miili ya raia wengine wa kigeni  ikiendelea kufanyiwa utaratibu wa kusafirishwa kuelekea katika nchi zao.


Miili hiyo ni pamoja na mwili wa aliyekuwa mkurugenzi wa YWAM Arusha Dkt John Mukolwe raia wa Kenya na Vicent kazungu ambaye alikuwa ni msajili wa wanafunzi katika taasisi hiyo ambaye ni mzaliwa wa Mwanza.


Akiongoza zoezi hilo mkurugenzi wa shirika la YWAM Tanzania Jeremiah Kiwinda aliishukuru serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu kwa msaada walioutoa tangu ajali hiyo ilipotokea ikiwemo majeruhi wa ndani na nje ya nchi kupatiwa matibabu bure.


“Rais Samia alielewa maumivu ya watu, 

alilivaa jambo hili kama mama amekuwa mfariji wetu na majeruhi wote wa ndani na nje ya nchi wanaendelea na matibabu bure  lakini pia kushiriki kikamailifu katika taratibu za kusafirisha miili ya wenzetu wa mataifa mbalimbali waliofariki katika ajali ile, Mungua ibariki Tanzania,” Alisema Jeremiah


Alieleza  kuwa msiba huo umewaumiza sana kwani waliondoka ni viongozi wanaowategemea na sio rahisi kupata mbadala wao kwasababu kila mmoja anafanya kazi kwa wito wake ambao sio wa kufundishwa hivyo imekuwa ni ngumu na pigo kubwa kwao.


Alifafanua kuwa waathirika wa ajali hiyo waliokuwa katika gari la shule ya New Vision wakiwemo majeruhi na waliofariki walikuwa katika mafunzo ya kupata shahada ya uongozi (PHD) inayotolewa na chuo cha kimisioni kinachoitwa university of the nations ambacho kipo ndani ya shirika la YWAM Duniani ambapo kwa mwaka huu mafunzo hayo yalikuwa yakitolewa YWAM Arusha.


“Walipata ajali wakiwa wanatoka katika ziara ya mafunzo ambayo ilikuwa ni kwenda kukutana jamii kuona na kujua hali halisi iliyopo  ambapo walienda katika kituo chetu kingine Longido, Engikaret na wakati wanarudi ndipo ajali hiyo ikatokea na miili ya raia wengine wa kigeni bado ipo mochwari tukiendelea na taratibu za kusafirisha kwani kunahitajika fedha kwaajili ya zoezi hilo lakini pia vibali,” Alisema Jeremiah.


Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Arumeru Emmanuela Kaganda alisema kuwa amevutiwa sana na wananchi wa wilaya hiyo katika eneo hili la Ngaramtoni kwani kwani baada ya kutokea kwa ajali hiyo walifanya kazi kubwa ya kusaidia majeruhi na kuweka ulinzi  kabla ya serikali kufika.


“Maeneo mengi  kunapotokea tukio kama lile kuna watu wenye nia ovu ambao wanakuwepo kwaajili ya kufanya uhalifu lakini watanzania wengi wenye nia njema walikuwa pale kusaidia tunawashukuru sana,” Alisema 


Aliendelea kusema kuwa serikali itaendelea kushitikiana nao bega kwa bega kuhakikisha majeruhi ambao wapo hosipitali wanaendelea kupata matibabu stahiki na bure kama ilivyoelekezwa na Rais wa jamuhuri ya muungano wa tanzania lakini pia kuhakikisha vibali na taratibu zingine za kusafirisha miili ya raia wa kigeni kwenda katika nchi zao zinakamilika hivyo taasisi ya hiyo isisite kuwasiliana serikali pale wanapokutana na changamoto zozote.


Naye  Salvatory Kalute afisa elimu wilaya ya Arusha alisema kuwa halmashauri imepoteza viongozi wazuri katika elimu ambao wamesimamia kwa umahiri mkubwa shule ya New Vision kwa kutoa elimu bora  amabpo walikuwa ni watu wanaoboresha elimu katika halmashauri hiyo na wamekuwa wakishirikiana katika kila hali kuimarisha elimu na michezo mbalimbali.


Mbunge jimbo la Arusha Magharibi Noah Lemburis alieleza walikuwa pamoja kwaanzia taasisi hiyo ikianzishwa na imekuwa ni sehemu kubwa  ya maendeleo katika jamii,wilaya na mkoa kwa ujumla kwani wamekuwa wakijishughulisha katika kutoa huduma mbalimbali kwa jamii ikiwemo elimu.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI