Na Mbaruku Yusuph Matukio Daima APP, Lushoto.
CHAMA cha Wananchi CUF kimeendelea kupata mtikisiko kutokana na Vigogo wa chama hicho kuendelea kutimkia katika Chama cha Mapinduzi.
Jana Februari 4,aliyekuwa mgombea wa Ubunge katika Jimbo la Kisarawe Rashid Mwishehe almaarufu kama 'KINGWENDU' alifanya maamuzi magumu ya kutimkia CCM kwa kile anachodai kumuunga mkono Mwenyekiti wa chama hicho Taifa Dr Samia Suluhu Hassan.
Kingwendu alitangaza kuhamia CCM katika mkutano wa hadhara wa kusherekea miaka 47 ya kuzaliwa kwa chama hicho, Sherehe hizo zilizofanyika katika viwanja vya michezo vya Shule ya Msingi Mbwei Wilayani Lushoto mkoani Tanga.
Kingwendu alisema, ameamua kuhamia CCM kutokana na chama alichokuwa nacho awali kukosa mvuto wa kisiasa na dira inatakayowaongoza katika mapambano ya kisiasa.
"Nimerudi nyumbani ,huko nilikokuwa hakuna mvuto kabisa, nilikuwa namiliki magari mawili lakini yote nimeuza kwa ajili ya kusaidia chama,naombeni mnipokee na mnisapoti "Alisema Kingwendu.
Kingwendu alikuwa kivutio katika mkutano huo ,ikumbukwe kuwa alipokuwa CUF aliwahi kugombea Ubunge Jimbo la Kisarawe mwaka 2015, alichuana na Suleiman Jafo ,na mwaka 2020 aligombea Ubunge Jimbo la Ilala huku ikielezwa kuwa alikisumbua Sana chama cha mapinduzi kutokana na kuwa na ushawishi mkubwa katika jamii.
Akimpokea mwanachama huyo mpya,Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Tanga Rajab Abdalah, alisema wamempokea mwanachama huyo mpya kwa moyo wote na kuahidi kumpa ushirikiano,
"Karibu katika chama cha ushindi,hapa umefika sehemu salama,tunakuahidi kukupatia ushirikiano wote" Alisema Rajab.
0 Comments