Na Ibrahim Yassin.Matukio Daima App.Songwe.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Songwe kimesema mwanachama anayetangaza nia kuwania uongozi kabla ya muda kuelekea uchaguzi serikali za mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu 2025 anapoteza sifa ya kuwa mgombea.
Hayo yamesemwa leo Februari 25,2023 na mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo Radwello Tullo Mwampashi wakati akizungumza na wanachama wa Chama Cha Mapindu zi wilaya ya Ileje akiambatana na wajumbe wa kamati ya siasa na wajumbe wa sekretalieti ya mkoa kwa lengo la kukijenga chama kuelekea uchaguzi ujao.
Mwampashi amesema Chama hicho kinaamini katika umoja na mshikamano na kwamba wanaotangaza nia mapema kutaka uongozi hususani Udiwani na Ubunge kabla ya muda wamepoteza sifa kwa kuwa wanakigawa chama.
"Suala hili lipo wazi katika chama chetu, wafahamu wazi viongozi wenye sifa waliowahi kuongoza nchi hii hawakujitangaza mapema walisubiri na muda ulipofika walitangaza nia ya kuwania hivyo hatutamwonea mtu kukata jina lake," amesema Mwampashi.
Kwa upande wake mjumbe wa halmashauri kuu ya chama hicho mkoani humo Adeni Mwakyonde amewasihi wenye nia ya kugombea wasubiri utaratibu wa chama utakapotolewa ikiwepo miongozo ya uchaguzi muda utakapofika.
"Wapeni ushirikiano viongozi waliopo madarakani watimize majukumu kusimamia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi mwaka 2022-2025 kwa kuwaletea wananachi maendeleo," amesema Mwakyonde.
Mwanachama wa chama hicho Rewardi Songa amesema viongozi waliopo madarakani wanahofu ya kuongoza kutokana na makundi mbalimbali ya wanaotia nia kuwachafua hivyo kutaka chama kitoe maelekezo ili kuwapa nafasi viongozi waliopo madarakani kuongoza kwa amani.
Elizabeth Kashililika amesema viongozi wapewe nafasi ya kuongoza kwa muda wa miaka mitano hivyo wanaojitokeza kabla ya muda vikao vya chama visiwape nafasi ya kugombea.
Katika kikao hicho jumla ya wanachama 20 wamejiunga Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka vyama vya upinzani ikiwepo Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Civil United Front (CUF)
0 Comments