Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Mahakama ya hakimu mkazi wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma imemuhuku kifungo cha miaka 30 gerezani dereva boda boda Ruben Gerishon (24) mkazi wa Kijiji cha Mlela wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumbaka msichana mmoja ambaye alikuwa abiria wake.
Boda boda huyo pamoja na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 gerezani pia mahakama ya Hakimu Mkazi wilaya ya Uvinza imetaifisha pikipiki iliyokuwa ikitumiwa na mshitakiwa huyo na kwa sasa imekuwa mali ya serikali.
Akitoa hukumu ya kesi hiyo Hakimu Mkazi wa mahakama ya wilaya Uvinza, Misana Majura aliiambia mahakama hiyo kwamba amejiridhisha pasi na kutia shaka kwamba kulingana na Ushahidi ulitolewa mahakamani hapo umethibitisha mshitakiwa kuwa alitenda kosa hilo.
Hakimu majura katika hukumu yake alisema kuwa mshitakiwa anastahili kupata adhabu kali kulingana na kosa alilotenda ili iwe fundisho kwa watu wengine ambao wanania ya kutenda kosa kama hilo na kwamba makosa hayo yamekuwa yakisababisha madhara makubwa kimwili na kiakili kwa waathirika.
Awali mahakamani hapo Mwendesha mashitaka wa polisi aliieleza mahakama kwamba Septemba 7 mwaka jana Mshitakiwa alikodiwa na msichana mwenye miaka 24 ili ampeleke Kijiji cha Kidahwe kutokana na wakati huo kutokuwepo kwa usafiri mwingine.
Mshitakiwa akitumia pikipiki yenye namba za usajiili MC 601 DLB aina ya King Lion alikubali ombi la msichana huyo na ndipo walipofika njiani akatekeleza unyama huo.
Mwendesha mashitaka huyo aliieleza mahakama ya Hakimu Mkazi wilaya ya Uvinza kuwa mshitakiwa alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Septemba 11 mwaka jana na kusomewa shitaka lake na ndipo hukumu ilipotolewa wiki hii.
Mwisho.
0 Comments