Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Mkuu wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye amewaonya watendaji wa serikali mkoani humo kutumia magari yanayotolewa kutumika kwa malengo ya kuboresha utoaji huduma kwa wananchi badala ya magari hayo kutumika kuzunguka nayo kwenye maeneo ambayo hayako kwenye taratibu zilizopangwa na ofisi
Mkuu huyo wa mkoa alisema hayo akikabidhi magari saba aina ya Toyota Hard Top yatakayotumika kwa ajili ya mpango wa usimamizi shirikishi wa sekta ya afya unaolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi kwa urahisi ili kutoa huduma za uhakika na za kuaminika.
Magari hayo saba yanaufanya mkoa Kigoma kupokea jumla ya magari 15 ambapo awali yaliyotolewa magari manane ya kubebea wagonjwa (Ambulance) yaliyotolewa na Raisi Samia Suluhu Hassan katika mpango wake wa kuboresha sekta ya afya nchini.
Andengenye alisema kuwa serikali imetumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ununuzi wa magari hayo kutokana na mahitaji yanayolenga kuimarisha utendaji wa wataalam na watumishi wake, kutokana na hilo ameonya kuwa ofisi yake haitakubali kuona magari hayo yanatumika holela kwa kazi ambazo ziko nje ya utaratibu wa ofisi.
Awali Katibu Tawala wa mkoa Kigoma, Albert Msovela alisema kuwa magari hayo saba yatakwenda kwenye mamlaka za serikali za mitaa kwa ajili ya usimamizi kwenye sekta ya afya ikiwemo ofisi ya Katibu Tawala wa mkoa (kwa RMO), Hospitali ya rufaa ya mkoa Kigoma Maweni,Halmashauri ya wilaya Buhigwe,Kibondo,Kasulu Mji, Halmashauri ya wilaya Uvinza na Chuo cha Waganga Maweni mjini Kigoma.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa mkoa Kigoma,Dk. Jesca Leba alisema kuwa tayari ofisi yake imeshapokea magari manane ya kubebea wagonjwa (Ambulance) ambayo yameshapelekwa kwenye vituo vilivyolengwa na yameanza kutoa huduma na kwamba magari haya saba ya awamu ya pili yatawasaidia katika kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa huduma za afya mkoani humo.
0 Comments