Header Ads Widget

RAIS OTHMAN ATAKA MISWADA YA SHERIA IENDANE NA MAONI YA WANANCHI

  

Na Fatma Ally, Matukio DaimaApp, Dar 

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Othman Masoud Othman ameitaka Serikali kufanya mabadiliko ya sheria za uchaguzi ili kuimarisha uwajibikaji wa viongozi na kuhakikisha maoni ya wananchi yanasikilizwa.


Aidha, ametaka maoni ya wananchi yanayotolewa kuhusu miswada ya sheria za uchaguzi inaendana na maoni yao.


Rai hiyo ameitoa jijini Dar es Salaam wakati alipokua akifungua mkutano maalum wa baraza la vyama vya siasa unaoshirikisha wadau mbalimbali wa demokrasia unaofanyika jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa  JNICC.


Amesema kuwa, lengo la mkutano huo ni kujadili na kutoa maoni ya miswada ya sheria za uchaguzi na muswada wa sheria za vyama vya siasa iliyowasilishwa bungeni Novemba 10, 2023, ambapo tayari Bunge limewaalika wadau mbalimbali kuwasilisha maoni na mapendelezo mbele ya kamati zake.


"Miswada hiyo ni ya sheria ya uchaguzi wa urais, ubunge na udiwani wa mwaka 2023, ambapo muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi wa mwaka 2023 na muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria za vyama vya siasa wa mwaka 2023"amesema Rais Othman.


Aidha, amewaomba wazee wenye uzoefu wa kada tofauti kusaidia kupata mwafaka wa kitaifa ili miswada ikienda bungeni, wabunge wapitishe jambo ambalo tayari lina mwafaka miongoni mwa viongozi wa kisiasa.


Katika hotuba yake, Othman amesema inawezekana baadhi wanaweza kuuchukulia utamaduni unaoendelea kujengeka wa kuwashirikisha wadau mbalimbali katika masuala yenye masilahi mapana ya kitaifa kama ni jambo tu la kawaida. 


Amesema utaratibu huo wa kukutana na kuzungumza, unatoa fursa kwa Watanzania kushirikishwa kupitia taasisi mbalimbali zinazowawakilisha.


"Hivyo sauti zao zimesikilizwa kupitia viongozi wao, ninawasihi sana na kwa heshima kubwa, mkutano huu uache alama ya utamaduni mwema wa majadiliano.


“Uwe mkutano wa utajiri wa mawazo ya washiriki na sio mkutano wa mapambio na kutimiza tu utaratibu tunaoanza kuuzoea wa kusema wadau walishirikishwa japokuwa kiuhalisia hawakusikilizwa," amesema.


Amesema kuna maoni mbalimbali amekuwa akiyasikia kuhusu miswada hiyo. Othaman ametolea mfano, “Nimesikia maoni ya watu wengi kuhusu usimamizi wa uchaguzi kuepuka wasimamizi wenye rekodi za kisiasa.


"Hili linaweza kuepukwa kwa kuweka vifungu bayana katika sheria vinavyokataza mtu yeyote ambaye ana rekodi ya kushiriki siasa waziwazi kwa kipindi fulani,  kutofaa kuwa msimamizi wa uchaguzi.


"Vilevile kwenye jopo la uteuzi wa Tume ya Uchaguzi, nimesikia maoni ya viongozi wa kisiasa kuwa na uwakilishi, hili ni jambo linalowezekana kwa kujadiliana namna bora ya kupata jopo la uteuzi bila ya viongozi wa kisiasa kutilia shaka, mwisho, nimesikia kilio cha muda mrefu cha vyama vya siasa kuhusu kanuni ya kukokotoa ruzuku kwa vyama," amesema.


Othman ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa chama cha ACT- Wazalendo, Zanzibar akifafanua suala la ruzuku amesema hilo linawezekana bila kuathiri kiwango cha bajeti ya ruzuku kwa kutekeleza mapendekezo ya Kikosi Kazi,  kwamba asilimia 10 ya bajeti ya ruzuku igawiwe kwa vyama vyote kwa usawa.


“Ni vyema tukumbuke miswada hii sio tu ya kurekebisha sheria bali ni sehemu ya kutekeleza maono mapana ya Rais Samia Suluhu Hassan ambayo wadau wengi wanayaunga mkono. Maono hayo ni  ya ujenzi wa Taifa yaliyojengwa katika 4R ambazo ni maridhiano, mageuzi, kujenga upya na ustahimilivu. 


Amesema kuwa, wanataka kufanya mageuzi katika suala la uwajibikaji ambapo hakuna budi kufanya mageuzi katika mfumo wao wa uchaguzi huku nchi ikiwa inahitaji bila kuchelewa ni kujenga misingi ya uwajibikani katika ngazi zote.


"Mageuzi ya kweli, mageuzi ya dhati yatakayozaa kilicho bora kwa Taifa letu na sio kilicho bora kwa wachache wanaofaidika na kukosekana kwa uwajibikaji katika Taifa, uchaguzi ndio unaozaa uongozi wa kitaifa na utendaji wa taasisi zote," amesema.



Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama amesema kuwa maoni yatakayochukuliwa na Serikali hayatachachuliwa yatakwenda kama yalivyo na kufikishwa sehemu husika.


"Maoni yatakayotolewa hapa yanawekwa sawa na kuwasilishwa mahali panapohusika bila kuchakachuliwa hili litakuwa ni jambo jema, hata Serikali ingependa kupata nafasi ya kujifunza kwa wadau, kusikia  wanafikiria nini katika kuimarisha demokrasia ndani ya Taifa letu.


"Serikali inaweza ikapata nafasi nzuri kwa sababu elimu haina mwisho kupitia maoni ya wadau na ushauri utakaotolewa katika mkutano huu, niwahakikishie wajumbe tutashiriki mkutano huu kwa siku zote mbili ili kuyachukua yote," amesema Mhagama.



Naye, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungia, amewaondoa hofu wadau kuwa maoni yao hayatachakachuliwa bali yatachukuliwa yote tena kwa kuandikwa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI