Na Pamela Mollel,Arusha
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki (Mb), ameongoza kiapo cha utii kwa Kamishina wa Uhifadhi - TANAPA, Musa Nassoro Kuji Juma katika hafla ya uapisho iliyofanyika leo tarehe 29,januari 2024 makao makuu ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania, jijini, Arusha.
Akizungumza baada ya uapisho huo Waziri wa Maliasili na Utalii alitoa maagizo 14 kwa Kamishna wa Uhifadhi Kuji ikiwemo kuhakikisha ulinzi wa maliasili unaimarishwa wakati wote, kusimamia na kufuatilia doria zifanyike ipasavyo ili kukabiliana na vitendo visivyofaa ndani ya Hifadhi Ikiwemo swala la Mifugo, na uchimbaji wa madini.
Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt.Hassan Abbas alisisitiza kufanya kazi kama timu na kubainisha kuwa kila nafasi inakuja na majukumu yake.
“Nafasi hizi zinakuja na majukumu yake, “Team work” ni muhimu sana. Nikuhusie sana, TANAPA ni taasisi kubwa sana nchini na duniani, shirikianeni na sisi wizara tutakuwa tayari kushirikiana na wewe. Mtegemee Mwenyezi Mungu katika majukumu yako ”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini -TANAPA, Jenerali (Mstaafu) George Waitara alimpongeza Kamishna Kuji kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Kamishna wa Uhifadhi TANAPA.
“Binafsi sina mashaka na uzoefu wako ndani shirika wa miaka 33 ni matumaini yangu uzoefu huo utatumia katika kukuza uhifadhi na utalii katika shirika na kuendelea kufanya vizuri katika ngazi za kimataifa”.
Kamishna wa Uhifadhi - TANAPA Mussa Nassoro Kuji Juma ameahidi ushirikiano na watumishi wote kuhakikisha wanalinda urithi wa maliasili zilizopo nchini sambamba na kufanya kazi kwa bidii na nidhamu.
“Awali ya yote namshukuru Mungu kwa tukio hili la kuvishwa vyeo, pili nimshukuru Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniteua kuwa Kaimu Kamishna na baadae kuwa Kamishna wa uhifadhi wa TANAPA “ alisema Kamishna Kuji.
Aidha, Kamishna Kuji alisisitiza ushirikiano kwa watumishi ili kufikia adhma ya serikali ya kuanzisha taasisi hii na kuahidi kusimamia maeneo yote ya hifadhi kikamilifu.
Kamishna Musa Nassoro Kuji Juma amechukua nafasi ya Kamishna wa TANAPA, William Mwakilema ambaye sasa ameteuliwa na Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa wilaya ya Korogwe.
0 Comments