Na Thobias Mwanakatwe, MKALAMA
WILAYA ya Mkalama mkoani Singida imeadhimisha miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika kwa viongozi kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwamo kupanda miti zaidi ya 700 katika kituo cha polisi cha wilaya hiyo pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Mkalama.
Akizunguma leo Disemba 9, 2023 mara baada ya kuhitimisha zoezi la upandaji miti , Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Moses Machali amewataka wananchi pamoja na watumishi kuwa wazalendo kwa nchi yao, kujituma na kuwajibika kufanya kazi kwa bidii kwa masilahi mapana ya nchi yao.
“Hatuwezi kupata maendeleo kama hatufanyi kazi, juzi Mkuu wa Mkoa wa Singida,Peter Serukamba ametuelekeza kuwa njia pekee ya kuhakikisha tunapata maendeleo ni kufanya kazi, kila kaya inakuwa na angalau ekari mbili, katika msingi huo tunaweza kuleta mabadiliko ambayo tunahitaji," amesema na kuongeza “leo tumepata Uhuru wewe ambaye ni mtumishi wa serikali, mtumishi katika 'private sector' unapokuwa unafanya kazi je, masaa yote ambayo umepangiwa kufanya kazi unayatumia vizuri kuweza kuzalisha kwa ajili ya taifa lako? Watu tumepata uhuru lakini tunauchezea, watu wanafanya uhuni mahali pakazi, ubadili tabia zetu, tuwajibike ili tuweze kusukuma maendeleo ya taifa letu," amesema.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkalama, Peter Masindi, aliwataka wananchi kuendelea kudumisha amani iliyopo nchini sambamba na kuendelea kuienzi siku hii muhimu ya Uhuru kwa watanzania katika kuwakumbuka wazee, viongozi waliojitolea kwa ajili ya uhuru wa taifa la Tanganyika.
“Leo ndio tarehe yetu ya kupata Uhuru, tumefanya hili tukio kwa ajili ya kukumbushana kwamba tuliumia, waliumia na sisi tuumie kwa ajili ya wengine,tusiache hii tarehe ikapita kama ilivyokuja, tarehe itabadilika, lakini maendeleo na amani ya nchi yetu tuendelee kudumisha,” alisema.
Maadhimisho haya yaliambatana na uzinduzi wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025-2050 ambapo kauli mbiu ya uhuru mwaka huu ni Miaka 62 ya Uhuru umoja na mshikamano ni chachu ya Maendeleo ya Taifa letu.
0 Comments