NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR
WAZIRI wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dk. Saada Mkuya Salum, amesema ujio wa taasisi ya uhasibu Tanzania (TIA) Zanzibar utasaidia kuinua kiwango cha elimu ya uhasibu nchini.
Aliyasema hayo alipokuwa akizindua kampasi ya saba ya Chuo hicho, Tawi la Zanzibar huko katika jengo la Thabit Kombo Mjini Unguja, alisema, mahitaji ya elimu yapo mengi kwa sasa hivyo kuja chuo hicho kutasaidia kukidhi mahitaji hayo.
Alisema kuongezeka kwa mahitaji ya kielimu nchini kumesaidia kwa kiasi kikubwa kuongezeka Taasisi za elimu ya juu Zanzibar.
Aidha alisema hatua hiyo ni ya kupongezwa na itafikia matarajio ya Serikali katika kuongeza wataalamu katika sekta muhimu nchini.
Alisema ufunguzi wa Tawi hilo umekuja wakati sahihi hasa ukizingati kuna watumishi wengi wenye vikwazo vya kufuata masomo nje ya Zanzibar.
Hivyo, alisema kuwepo kwa Chuo hicho kutarahisisha sambamba na kutumia muda baada ya kazi kuendelea na masomo kupitia taasisi hiyo.
Hivyo, alisema serikali ya mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Taasisi hiyo ili kuona wanatoa wasomi waliokuwa na viwango vizuri.
Sambamba na hayo, Waziri Mkuya aliuomba uongozi wa TIA kufungua kampani nyengine katioka kisiwa cha Pemba ili wananchi waliowengi waweze kufaidia na kada hiyo.
Nae, Afisa Mtendaji Mkuu wa (TIA) Profesa, William Ballargyo, alipongeza serikali kwa mashirikiano uliokuwepo baina yao na kuahidi kuweka vipaumbele muhimu katika udahili ili kuona wenye sifa wanapata fursa ya kujiunga na kampasi hiyo.
Alisema serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imetenga jumla ya shilingi bilioni tatu kupitia wizara ya fedha kwa ajili ya hatua ya awali za Ujenzi.
Akizungumzia mpango wa baadae wa Chuo hicho, Meneja Mmiliki wa Taasisi hiyo, Mhandisi, Masuhuko Nkuba, alisema wanatarajia kujenga majengo yao ya kudumu katika Kijiji cha huko Nganani makunduchi ambapo kwa hatua ya mwanzo wataanza na jengo litakalochukuwa wanafunzi elfu moja
Taasisi ya uhasibu Tanzania (TIA) kwa sasa inaedesha masomo hayo katika jengo la Thabit Kombo katika masomo mbali mbali yakiwemo Uhasibu,Ugavi na Teknolojia ya habari na Manunuzi.
0 Comments