Header Ads Widget

JAMII YATAKIWA KUPINGA MIMBA ZA WASICHANA WADOGO

Hery Lugala Afisa Miradi wa UNFPA mkoa Kigoma
Lucy Mabada Mkunga Mshauri kutoka Chama Cha Wakunga Tanzania (TAMA)
Neema Boniface mmoja wa wasichana walioathirika na mimba za utotoni wilayani Kasulu

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

Ili kiwalinda wasichana wadogo na  changamoto ya mimba za utotoni  jamii mkoani Kigoma imetakiwa  kushirikiana na wadau katika kutekeleza mikakati ya kukabiliana na changamoto hiyo.

 

Afisa Miradi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu (UNFPA) kwa mkoa Kigoma,Hery Lugala  alisema hayo katika Kijiji cha Muzye wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wakati wa tamasha la kutoa elimu na kuhamasisha jamii kupinga vitendo vya ukatili kwa wasichana kuelekea maadhimisho ya siku ya kupinga ukatili duniani.

 

 Lugala alisema kuwa mimba kwa wasichana wadogo zinaharibu ndoto na mipango yao mbalimbali ikiwemo ya elimu ambapo alisema kuwa serikali,wadau na jamii wakiungana wanaweza kuwapa uelewa wasichana wadogo kujikinga na vishawishi na mambo yanayosababisha kuingia kwenye janga hilo.

 

“UNFPA katika kusimamia miradi ya mbalimbali ikiwemo afya, afya ya uzazi na ukatili itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kunusuru mabinti kwa kutoa elimu na kuboresha miundo mbinu ya utoaji huduma vituo vya afya  ili waweze kutimiza ndoto zao za kupata elimu lakini kuwa na mipango mingine ya maisha kwa siku za baadaye,”Alisema Afisa Miradi huyo.

 

Akizungumza katika tamasha hilo Mkunga Mshauri kutoka chama cha Wakunga Tanzania (TAMA),Lucy Mabada  ambacho kinaendesha mradi wa kuwasaidia wasichana wadogo waliopata ujauzito (Mama Wadogo) alisema kuwa elimu ndiyo nguzo muhimu kwa ajili ya kuwakinga mabinti wadogo kuingia kwenye changamoto ya kupata ujauzito.

 

Mabada alisema kuwa katika kutimiza hilo tayari wameshatoa mafunzo kwa waelimishaji rika ngazi ya jamii 55 ambao wanabeba jukumu kubwa la kufundisha jamii madhara ya wasichana wadogo kupata ujauzito na kwamba tangu mwaka 2018 kata 18 za mkoa Kigoma zimefikiwa na elimu hiyo.

 

Mmoja wa wasichana waliothirika na ujauzito katika umri mdogo,Neema Boniface  ambaye ni miongoni mwa wasichana wanaotekeleza mradi huo wa TAMA alisema kuwa kutokuwa na elimu ya afya ya uzazi kwa mabinti,  umasikini wa wazazi na tamaa ya mabinti imekuwa changamoto kubwa inayofanya mabinti kutumbikia kwenye changamoto hiyo na kuharibu Maisha yao.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI