Na Thobias Mwanakatwe, MKALAMA
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama limewachukulia hatua watumishi nane wa halmashauri hiyo baadhi yao kwa kufukuzwa kazi kutokana na tuhuma mbalimbali ikiwamo kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kutokana na ulevi uliokithiri.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, James Mkwega alitangaza maamuzi yaliyofikiwa na baraza hilo juzi wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani kilichoketi kwa ajili ya kujadili utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024.
Aliwataja waliofukuzwa kazi kuwa ni wauguzi wawili ambao ni Antonia Atanasi ambaye ni Mtabibu msaidizi Zahanati ya Mziba na Mary Kingu ambaye ni muuguzi wa Zahanati ya Iguguno.
Watumishi hao wamechukuliwa adhabu hiyo kutokana na kosa la utoro kazini kwa zaidi ya siku tano bila taarifa ya mwajiri.
Mkwega aliwataja watumishi wawili waliochukuliwa adhabu ya kukatwa mshahara kwa asilimia 15 kwa muda wa miaka mitatu kutokana na ulevi uliokithiri kuwa ni Kelvin Nyachi ambaye ni Afisa Manunuzi msaidizi Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama na Farida Mathias Kigaila ambaye ni mteknolojia mwandamizi wa maabara katika Hospital ya Wilaya ya Mkalama.
Watumishi wengine waliopewa barua ya onyo kwa kosa la kukiuka taratibu za fedha na manunuzi ni Ismail Tundu ambaye ni Afisa mtendaji kijiji na Daudi Mazengo mtendaji wa Kijiji cha Manyongo.
Mwenyekiti huyo alimtaja mtumishi mwingine aliyechukuliwa hatua ni Mtatiro Galache ambaye Mteknolojia wa dawa kituo cha afya Nyabuli aliyepewa adhabu ya kukatwa mshahara kwa asilimia 15 kwa muda wa miaka mitatu.
Mtumishi mwingine Mizungu Macheli Chazy Mtabibu msaidizi hospital ya Wilaya ambaye alikuwa akituhumiwa kwa ulevi,Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama liliamuru tuhuma zake zichunguzwe upya.
Mkwega akizungumza baada kusoma maamuzi hayo ya baraza, aliwataka watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama alisema madiwani hawafurahii kumwita mtumishi kwenye Kamati ya Uongozi kuhojiwa kwa ya ulevi.
Alisema watumishi wazitendee haki nafasi zao kwani wapo watu ambao wameenda kwa waganga wa kienyeji na wengine kwenda na udongo na maji kuombewa ili wapate nafasi za kuteuliwa lakini hawakufanikiwa.
"Mwaka 2014/2015 haikutokea kujadili mtumishi yeyote kwenye Kamati ya Uongozi lakini leo hii inatokea mtumishi anajadiliwa kunywa pombe halafu pombe kwanza haijakatazwa kunywa kinachotakiwa usinywe pombe wakati wa kazi," alisema.
0 Comments