Header Ads Widget

ASILIMIA 54.8 YA WATU MKOA WA ARUSHA NI TEGEMEZI

NA MAMNYAK KIVUYO, ARUSHA 

kati ya watu milioni 2.4 wa mkoa wa Arusha asilimia 49.6 ni watoto waliochini ya miaka 18 na asilimia 5.2 ni wazee wenye umri wa miaka 60 kuendelea idadi inayoufanya mkoa kuwa na kundi kubwa tegemezi.

Akitoa mafunzo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi 2022 yaliyotolewa kwa viongozi na watendaji, halmashauri na wadau mbalimbali wa mkoa wa Arusha Mtakwimu kutoka ofisi ya mtakwimu mkuu Dodoma Dkt Omary Mwinyi alisema kuwa katika watu 100 waliopo katika umri wa kufanya kazi wanategemewa na watu 81.

“Kuna kuna haja kubwa ya viongozi kutengeneza fursa za ajira ili walio katika umri wa kufanya kazi waweze kulimudu kundi tegemezi lililo nyuma yao kwani vijana ni asilimia 35.5  tu ya watu wote wa mkoa wa Arusha” Alisema Dkt Mwinyi

Aidha alifafanua kuwa kwa mujibu wa matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 mkoa wa Arusha unaonyesha kuwa asilimia 40.7 ya kaya zote  615,182 zinaongozwa na wanawake.

Dkt Mwinyi alisema kuwa mkoa wa Arusha una idadi  ya watu milioni 2.4 ambapo inachangia asilimia 3.8 ya watu wote waliohesabiwa lakini pia asilimia 3.3 ya ongezeko la watu ikiwa ni pamoja na kuwa na idadi kubwa ya wanawake ambapi kwa kila wanawake 100, wanaume ni 91.


“Kwa mkoa huu matokeo yanaonyesha kuwa wanawake wanaongezeka kwa kasi zaidi katika wilaya zote isipokuwa wilaya ya karatu pekee ambayo wanaume ni wengi kuliko wanawake ambapo kwa kila wanawake 100 wanaume 107, ” Alisema Dkt Mwinyi.


Alifafanua kuwa katika mkoa wa Arusha kaya  ni 615182 ambapo asilimia 40.7 zinaongozwa na wanawake huku wastani wa watu katika kaya ikiwa ni 4.3 na kuwataka watafiti waliopo mkoa wa Arusha kufanya utafiti kujua  nini sababu ya kaya hizo kuongozwa na wanawake peke yao.

Kwa upande wake katibu tawala msaidizi wa mkoa wa Arusha anayeshughulika na rasilimali watu David Lyamongi akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya mkuu wa mkoa John Mongela alisema kuwa matokeo ya sensa ni nyenzo nzuri katika kutunga sera ambazo zitaenda kuleta matokeo chanya katika maisha ya wananchi.

Alisema kuwa nchi kwa sasa inatekeleza tafiti tatu  za takwimu zinazofanyika nchi nzima ikiwemo mkoa wa Arusha ambazo ni tafiti za shughuli za  kiuchumi na kijamii, utafiti wa kilimo pamoja na utafiti wa upatikanaji endelevu wa huduma za maji, elimu ya afya na usafi wa mazingira ambapo tafiti hizo ni muhimu kwani zinaifanya nchi kupata takwimu rasmi zitakazo tumika kutunga na kuhuisha sera, kupanga mipango na programu za maendeleo.


Naye Mbunge wa viti maalum mkoa wa Arusha Zaytuni Sawai alisema kuwa katika mafunzo hayo wamejuisha wilaya tatu ambazo ni Arusha jiji, Arusha Dc na Meru na watarajia kufikisha elimu hiyo katika wilaya zingine zilizobaki kwani zoezi la sensa haliishii kwenye kuhesabu tu bali kwenye kupata takwimu sahihi.

“Tumieni takwimu hizi kufanya mipango kujua wenye uhitaji ni wangapi katika halmashauri na kata zetu kwani takwimu hizi ndizo zitakazo waletea maendeleo,” Alisema.

Hata hivyo idadi ya watanzania wote ni Milioni  61,741,120, wanaume wa kiwa ni milioni 30,053,130 sawa na asilimia 47.7 na wanawake wakiwa milioni 31,687,990 sawa na asilimia 51.3 huku uwiano wa kijinsia ukiwa ni  95 na kasi ya ongezeko la watu kutoka 2012 hadi 2022 kuwa ni asilimia 3.2

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI