Na Fadhili Abdallah, Kigoma
KIONGOZI Mkuu wa chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe ameanza ziara ya siku nane katika majimbo yote ya mkoa Kigoma akianzia ziara yake kwenye kijiji cha Ilabiro wilaya ya Kakonko mkoa Kigoma ambapo kulitokea kifo cha utata cha mwananchi wa kijiji hicho Enos Elias na kuitaka serikali kuchukua hatua kwa wote waliohusika na kifo hicho..
Akiwa katika siku yake ya kwanza ya ziara hiyo Kabwe alitembelea familia ya Enos Elias kwa ajili ya kutoa pole na kuwafariji wazazi na ndugu wa familia hiyo ya marehemu.
Marehemu Enos alikamatwa na idara ya uhamiaji wilaya ya Kakonko Oktoba 27 mwaka huu kwa madai ya kuwa na utata wa uraia na baadaye kuhifadhiwa kituo cha polisi Kakonko ambapo Oktoba 29 jeshi la polisi lilitangaza kutoweka kwa mtu huyo hadi wiki moja baadaye ilipokutwa maiti yake ikiwa imezikwa kwenye pori la kijiji cha Chilambo.
Kufuatia hali hiyo Kabwe alisema kuwa ameongea na Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Hamad Masauni akiitaka serikali kufanya uchunguzi wa kina kubaini kilichotokea na kuchukua hatua kwa wote waliohusika na kifo hicho.
Kabwe ameihakikishia familia hiyo kuwa watulivu wakati huu ambapo serikali na watetezi wa haki za binadamu wakichukua hatua kuhusika na kilichotokea na kwamba watahakikisha wanasimamia haki kutendeka.
Tayari Mkuu wa jeshi la polisi nchini, Camillius Wambura kupitia taarifa ya msemaji wa jeshi hilo, David Misime alisema kuwa polisi kwa kushirikiana na wadau wa haki jinai wameanza uchunguzi wa tukio na kutaka mtu yeyote mwenye habari na maelezo kuhusiana na kadhia hiyo kuiwasilisha kwa tume hiyo.
Katika hatua nyingine Kaimu Mkuu wa mkoa Kigoma, Mwanamvua Mrindoko ameunda kamati ya watu sita kuchunguza kifo hicho cha utata cha Mfanyabiashara huyo wa Katoro mkoani Kigoma Mwenyeji wa kijiji cha Ilabiro wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma.
Mwisho.
0 Comments