Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendot Zitto Kabwe amewaonya watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama hasa uhamiaji mkoani Kigoma kuacha kunyanyasa na kuwasumbua wananchi wanaofanya biashara kati ya Tanzania na Burundi kwa kigezo cha kuwa wahamiaji haramu kwani alisema kuwa jambo hilo linaweza kuvuruga biashara ya ujirani mwema na shughuli za uchumi ambazo viongozi wa nchi hizo mbili wameridhia
Zitto alisema hayo akihutubia mkutano wa hadhara kwenye kijiji cha Mnanila wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma kuwa Tanzania na Burundi ni nchi ambazo viongozi wake wameamua kufanya biashara na shughuli za kiuchumi kwa kutumia itifaki ya Jumuia ya Afrika Mashariki hivyo suala la uhamiaji lisiwe kikwazo cha kuvuruga shughuli za biashara na uchumi na kuwafanya watu wa maeneo hayo kuishi kama wako ukimbizi.
Sambamba na hilo Zitto ametaka kuharakishwa kwa ujenzi wa kituo cha pamoja cha forodha katika mpaka wa Tanzania na Burundi kijiji cha Mnanila tarafa ya Manyovu wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma akieleza kuwa kituo hicho ni muhimu katika kuchochea biashara kubwa na kuinua shughuli za uchumi baina ya nchi hizo.
Zitto amemtaka Waziri wa Fedha,Dk.Mwigulu Nchemba kuona umuhimu wa mradi huo kwani ni miaka saba sasa tangu wananchi waondolewe eneo hilo ili mradi uanze lakini hadi sasa mradi haujaanza na hakuna taarifa rasmi kwa wananchi kujua mradi huo utaanza lini.
Aidha Kiongozi huyo wa chama alisema kuwa lipo soko la ujirani mwema baina ya Wafanyabiashara wa Tanzania na Burundi ambalo limejengwa lakini bado soko hilo halina shughuli za kutosha za biashara na uchumi kwa sababu serikali haijaamua kwa dhati kutekeleza mkakati wa kiuchumi wa eneo hilo licha ya fursa kubwa ya wafanyabiashara na wajasiliamali kuwa nayo.
Akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini wa chama hicho, Muhonga Ruhwanya alisema kuwa pamoja fursa nyingi zilizopo baina ya Mpaka wa Tanzania na Burundi bado mpaka huo hauna shughuli za kutosha za biashara kutokana na serikali kuchukua muda mrefu kutekeleza mipango mikakati ya biashara na uchumi ya eneo hilo na kufanya eneo hilo kutokuwa na tija ya kutosha ya shughuli za biashara na uchumi.
0 Comments