Serikali ya Zambia imeondoa mafao ya kustaafu na marupurupu kutoka kwa Rais wa zamani wa nchi hiyo Edgar Lungu kutokana na uamuzi wake wa kurudi kwenye siasa.
Wiki iliyopita Mwanasiasa huyo alitangaza kurudi kwenye mapambano huku akisema “ ninarudi kupigania na kuilinda demokrasia ya nchi”.
Bw.Lungu alipoteza nafasi ya uongozi kwa Rais Hakainde Hichilema katika uchaguzi wa mwaka 2021, na baadaye alitangaza kustaafu.
Baada ya miaka sita ya kuiongoza Zambia, Lungu aliiacha nchi ikikabiliwa na hali ngumu kiuchumi huku ikiongoza kwa madeni barani Afrika.
Kurudi kwake kwenye siasa kunaashirikia mchuano mkali kwenye uchaguzi wa mwaka 2026.
Kama Rais mstaafu, alikuwa na haki ya kupewa maafisa watatu wa usalama, hati ya kusafiria ya kidiplomasia, magari matatu, nyumba iliyo tayari kuishi, bima ya afya,gharama zote za mazishi atakapofariki na kinga dhidi ya mashtaka.
Msemaji wa serikali hiyo Cornelius Mweetwa amesisitiza kuwa kuanzia sasa Bw.Lungu atachukuliwa kama raia mwingine yoyote.
0 Comments