Header Ads Widget

WAZIRI MKENDA ATAKA SOKO MAALUM LA KUUZIA KAHAWA YA ROMBO.

 


NA WILLIUM PAUL, ROMBO. 


WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ameitaka Bodi ya Kahawa nchini kwa kushirikiana na ofisi yake pamoja na wataalam wa zao la Kahawa katika jimbo la Rombo kutafuta soko maalum la uuzwaji wa zao hilo litakalomsaidia mkulima kuuza kwa bei nzuri. 


Profesa Mkenda ambaye ni Mbunge wa Rombo alitoa kauli hiyo jana wakati wa zoezi la ugawaji wa miche laki moja na elfu hamsini ya zao ambayo ni ya kisasa kwa wananchi wa jimbo hilo katika kijiji cha Kibaoni kata ya Nanjara. 



Alisema kuwa, wakulima wengi waliachana na kulima zao hilo kutokana na bei ya kuuzia kuwa ndogo ikilinganishwa na gharama wanazotumia kulima na kuudumia zao hilo. 


"Sasa hili watu wa Bodi ya Kahawa naomba tusaidiane na ofisi yangu kuhakikisha tunatafuta soko maalum ambalo tutakuwa tunaenda kuuza kahawa yetu ya Rombo haiwezekana mkulima wa kahawa pale Karatu auze kahawa kilo 24000-25000 alafu mkulima wa Rombo auze 3000-4000 kwa kilo tunataka kuitangaza kahawa yetu ya Rombo" Alisema Waziri Mkenda. 



Alisema kuwa, kwa sasa kahawa inayozalishwa Rombo ni tani 2000 lakini kutokana na miche hiyo iliyogawanywa kwa wakulima wanatarajia kuzalisha zaidi ya tani 4000 hali ambayo itasaidia kuleta maendeleo kwa wakulima. 


Aidha Mbunge huyo amewataka wakulima hao kupitia vyama vyao vya ushirika kutunza vizuri kahawa kwa kufuata maelekezo ya wataalam wa zao hilo ili kuzalisha kahawa iliyobora na kuweza kuitangaza kimataifa na kupata soko maalum. 



Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa, Kajiru Francis  alisema kuwa lengo la bodi hiyo ni kuongeza uzalishaji wa zao hilo ambapo serikali iliwawekea lengo la kuzalisha miche milioni 20 kwa kila mwaka kwa miaka mitano ifikie milioni 100.


Kaimu Mkurugenzi huyo alisema kuwa, kitalu cha Nanjara ni moja ya vitalo ambavyo vinazalisha miche hiyo ambapo kila eneo linalolimwa zao hilo kunakitalu cha miche. 



Alisema kuwa, miche hiyo hutolewa bure kwa wakulima kwa lengo la kuwapunguzia gharama za uzalishaji ambapo miche hiyo ni ya muda mfupi. 


"Zoezi la ugawaji wa miche katika wilaya ya Rombo linaendelea katika maeneo mengine kwani vipo vitalu vitatu vya kuzalisha miche" Alisema Francis. 


Aidha Kaimu Mkurugenzi huyo alitoa wito kwa wakulima kutambua kuwa serikali inatumia gharama kubwa kuzalisha miche hiyo na inatoa bure kwao ili iweze kuwazalishia na kuwataka kuitunza.


Naye Mtafiti wa usambazaji wa Teknolojia na mafunzo kutoka taasisi ya utafiti wa Kahawa nchini (TaCRI), Dkt. Jeremiah Magesa alisema kuwa, miche hiyo ya kahawa huchukua miezi 18 mpaka kuzaa kwake na kusisitiza wakulima kufuata kanuni za uzalishaji kahawa na Maafisa ugani kuwatembelea wakulima mara kwa mara na kuwapa ushauri. 


Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI