Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoa Kigoma imeweza kuwafikia wananchi 36,948 ambapo kati yao wanawake ni 17,553 kwa kuwapatia elimu kuhusu mapambano dhidi ya rushwa katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
Mkuu wa dawati la elimu kwa umma mkoa Kigoma,Leonida Mushama alisema hayo akitoa taarifa ya utekelezaji ya taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu Julai hadi Septemba mwaka huu kwa niaba ya Mkuu wa TAKUKURU mkoa Kigoma, Stephen Mafipa.
Kupitia elimu hiyo Mushama alisema kuwa TAKUKURU mkoa Kigoma imeweza kupokea jumla ya ya kero 117 zilizoibuliwa kwenye mikutano ya kata na wananchi katika program yake maarufu kama TAKUKURU RAFIKI.
Mushama alisema kuwa katika mikutano hiyo TAKUKURU mkoa Kigoma kupitia maafisa wake waliweza kutembelea jumla ya kata 15 za wilaya za mkoa Kigoma na kufanya vikao ambavyo vimefanikishwa kuibuliwa kwa kero hizo.
Afisa huyo wa dawati la elimu kwa umma alisema kuwa katika kero zilizotolewa sehemu kubwa zilikuwa zikihusu idara ya afya wananchi wakilalamikia upungufu wa watumishi na uhaba wa madawa,sekta ya elimu ambapo ilihusu upungufu wa walimu,ubovu,upungufu wa madawati na miundo mbinu duni ya shule.
Masuala mengine ni migogoro ya ardhi, umeme, malalamiko ya watumishi kutolipwa fedha za uhamisho na marupurupu mengine ambapo hadi sasa kero 70 zimetatuliwa na 47 zipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.
0 Comments