Header Ads Widget

WANAFUNZI: LRCT ANGALIENI SHERIA ZA KUBANA WASANII WANAOHAMASISHA DAWA ZA KULEVYA

Na Thobias Mwanakatwe

WANAFUNZI  wameiomba Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) kuangalia upya sheria inayowasimamia wasanii wa mziki wa kizazi kipya na watu maarufu ambao wanaimba nyimbo na  vitendo vinavyo hamasisha matumizi ya dawa za kulevya  ikiwemo bhangi pamoja na  ngono katika jamii za Watanzania.


Ombi hilo limetolewa na Wanafunzi wa kidato cha tano katika Shule za Sekondari za  Mazwi, Kizwite  na Kantalamba zilizopo Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa wakati wa tume hiyo ilipotembelea shule hizo  kutoa elimu ya sheria  kwa wanafunzi.

Katika taarifa  ya tume hiyo kwa vyombo vya habari jana, maombi ya wanafunzi hao yalitokana na mawasilisho ya sheria ya  kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya iliyowasilishwa na wakili Jackline Nungu na Sheria ya kanuni ya adhabu haswa katika masuala ya makosa dhidi ya maadili iliyotolewa na wakili wa Serikali  Dk. Kalekwa kasanga kutoka LRCT.


Wanafunzi hao wameeleza kwamba sheria inatakiwa kuangazia wote wanaochochea utendaji wa makosa kama hayo kupitia nyimbo zao au mavazi yenye picha za majani ya bhangi ili kusaidia vizazi vichanga kuepuka kufanya makosa hayo.



Awali Wakili Nyungu katika wasilisho lake alieleza kwamba Sheria ya  kudhibiti Dawa za  Kulevya ina mihimili mitatu  kwanza, kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya, pili kudhibiti biashara ya dawa za kulevya na tatu kudhibiti athari zitokanazo na matumizi ya dawa za kulevya .

Alisema sheria  hutoa adhabu kutokana na uzito kiasi cha dawa za kulevya ambapo adhabu ya kupatikana na kiasi kidogo cha dawa za kulevya ni kifungo cha jela kisichopungua miaka mitano au faini isiyopungua milioni moja au vyote kwa pamoja, wakati kosa la kupatikana na kiwango kikubwa cha dawa za kulevya kifungo ni kuanzia miaka 30 hadi kifungo cha maisha.



Katika hatua nyingine,Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) imejipanga kutoa elimu ya sheria kwa Wakurugenzi na Wakuu wa Idara katika halmashauri zote nchini ili kuongeza uelewa juu ya mabadiliko ya sheria mbalimbali .


Naibu Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Zainabu Chanzi, alisema hayo wakati akijibu maombi ya Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Mifugo katika Halmashauri hiyo, Tilinao Nsila.


Alisema kwamba moja ya majukumu ya Tume ya Kurekebisha Sheria  ni kutoa elimu ya sheria hivyo utekelezaji wa ombi hilo utaanza mara moja kuzingatia  bajeti pamoja na majukumu mengine ya tume.


Chanzi alibainisha kwamba  wakurugenzi na watumishi wengine ni wadau muhimu  hasa katika kipindi hiki ambacho taasisi inaendelea kukusanya maoni kwa ajili ya maboresho ya sheria mbalimbali.


"Katika halmashauri zetu Wakurugenzi ni wasimamizi muhimu wa Sheria hivyo inafaa wapewe elimu kuhusu utekelezaji wa sheria mbalimbali  ili   kupunguza utendekaji wa makosa katika Jamii" alisema.


Awali, Kaimu Mkurugenzi huyo alieleza kwamba sheria zinafanyiwa maboresho mara kwa mara  na kuna baadhi ya sheria ambazo hazifahamiki kwa watu na viongozi ambao ndio wanaosimamia utekelezaji wa sheria na maendeleo ya wananchi katika ngazi za halmashauri.


" Naomba elimu ya mabadiliko ya sheria mbalimbali zitolewe kwa Wakurugenzi na Wakuu wa Idara kwa kuwa itasaidia utoaji wa huduma kwa jamii kwa kufuata sheria,"alisema.


Katika  Mkoa wa Katavi wataalam kutoka tume hiyo walitoa elimu ya sheria ya makosa dhidi ya maadili,Sheria ya Kudhibiti  na  Kupambana na Dawa ya Kulevya, Makosa ya Kimtandao na Utakasishaji wa Fedha Haramu. Mafunzo hayo yalitolewa katika chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Mpanda, Chuo cha Sayansi na Maendeleo ya Jamii Mpanda,  vikundi vya waendesha bodaboda na bajaji, viongozi wa dini watendaji wa kata na wanawake wajasiriamali.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI