Header Ads Widget

WAFANYAKAZI WVC WACHANGIA DAMU, WAJA NA AINA 360 ZA MBEGU ZA MCHICHA

 


NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA

Kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Taasisi  ya utafiti na maendeleo ya mboga mboga Duniani kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika(World Vegetable Centre) wafanyakazi wake wameweza kufanya zoezi la kuchangia damu kwaajili ya kuokoa maisha ya watu wanaoweza kupoteza maisha kwa kukosa damu.


Hazina Iddi mmoja wa wafanyakazi wa Tasisi hiyo alisema kuwa alisukumwa kuchangia damu baada ya kupata elimu kuwa na yeye anaweza kuchangia kwasababu hana mahala panapo muuma na hakuna madhara  zaidi ni kusaidia kuokoa maisha ya watu mbalimbali wakiwemo waliopata ajali na kuvuja damu nyingi  lakini pia akina mama wanaojifungua.


“ Ni washauri Watanzania wenzangu kuacha kusikiliza uvumi uliopo katika jamii juu ya suala zima la uchangiaji damu kwani ni uzushi na hakuna mdhara, mimi nimechangia na sijapata madharayoyote na naendelea na kazi kama kawaida hivyo tuwe tayari kuchangia kwaajili ya msaada,” Alisema.



Mratibu wa Damu salama Wilaya ya Meru Abdalah Aziz alisema kuwa lengo la ukusanyaji wa damu ni ili kukidhi mahitaji katika wilaya yao ikiwa ni pamoja na kuhakikisha hakutakuwa na vifo vinavyotokana na ukosefu wa damu ambapo kwa mwezi wanatakiwa wakusanye uniti zaidi ya 150 ambapo kwa uchangiaji wa wafanyakazi wa tasisi hiyo wameweza kukusanya zaidi ya uniti 20.


Aidha kwa upande wa shughuli inayofanywa na Taasisi hiyo imefanikiwa kuja na aina 360 za mbegu za mchicha ambazo zinawapa watu fursa ya kuchagua kulingana na mahitaji ikiwemo aina zenye mbegu kwa wingi na zenye majani mengi.


Hayo yameelezwa na mtafiti  wa taasisi hiyo Omary Mbwambo wakati akiongea na waandishi wa habari walipofanya ziara kwenye mashamba ya kuzalishia mbegu za aina mbalimbali yanayosimamiwa na tasisi hiyo ambapo alisema kuwa katika tafiti zao wamelipa zao la mchicha kipaumbele kwani ni zao ambalo ni asili ya Afrika kutokana na kulimwa kwa muda mrefu.



Alisema kuwa kwenye mchicha watu wengi wanajua kuwa yanayotumika zaidi ni majani lakini kuna eneo muhimu kwa lishe  ambayo imesahaulika na ni mbegu ambapo Tasisi hiyo imeona kuna umuhimu wa kutafuta mbegu ambazo zitakuwa na tija kubwa kwa upande wa mbegu.


“ Kwasasa tunazo aina ambazo kama unataka majani tu itakupa tija zaidi  kwasababu ina kiwango kikubwa cha majani lakini pia tuna aina zenye  matumizi mawili ambayo unaweza ukala majani lakini pia ukapata mbegu, na kuna nyingine ambazo ni kwaajili ya mbegu zaidi,” Alisema.


“Kwenye mchicha watu wengi hasa Watanzania tunapenda yenye majani ya kijani lakini kuna soko lingingi hasa Uganda wao wanapenda zaidi mchicha mwekundu  kwahiyo tuna uwanda mkubwa kwa sasa wa kuweza kuchagua kulingana na uhitaji wa watumiaji husika kulingana na sifa wanazozihitaji,”. Alieleza.


Alifafanua kuwa kwenye Mchicha wamefika mbali kwa upande wa kuziboresha ambapo ili mbegu hizo ziweze kuwafikia wakulima wanashirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo kampuni za mbegu, vituo vya utafiti vya nchi mbalimbali kwa mfano kwa Tanzania wanayo taasisi ya kilimo ya TARI, pamoja na kampuni za mbegu zinazofanya kazi kikanda na kimataifa kwaajili ya kuzisajili na kuzisambaza.


Aliendelea kusema kuwa mbegu hizo baada ya mkulima kuzipata anaweza kujizalishia mbegu zake mweyewe jambo ambalo linafanya mbegu hizo kukosa msukumo  kwenye soko katika kampuni zinazofanya kazi kibiashara kutokana na baada ya kumuuzia mkulima kutorudi kwasababu tayari atakuwa anazalisha mbegu zake mwenyewe.


Kwa upande wake Dkt Sognigbe N'Danikou mwanasayansi mtafiti wa mbegu za asili za mboga mboga  kutoka Tasisi hiyo alisema kuwa kituo hicho ni ufunguo wa mkusanyiko wa mbegu za asili Afrika ambapo lengo lao ni kukusanya na kuzifanyia tafiti na kuziboresha na kuzihifadhi sio tu kwaajili na kilimo na lise lakini pia kwaajili ya vizazi vijavyo.


“Tumekusanya mbegu zaidi ya elfu 6000 za mbogamboga na katika hizo tumeweza kuzifanyia tafiti na kuziboresha ambapo kutokana na mbegu hizo sasa tumeweza kuzalisha mbegu mpya zaidi ya 100 ambazo ni rafiki na hizo zikiwemo za mchicha, N'gogwe, Mnavu na nyinginezo ambazo tunaziita ni mbegu za asili za Afrika,” Alisema.


“Tunapokea mbegu kutoka kwa wakulima kutoka maeneo tofauti ikiwemo Tanzania, Uganda, Kenya, Madagascar, Benin, Senegal na nchi zingine zinakuja katika kifungashio kidogo sana ambapo tunachokifanya ni kuziendeleza kwa kuzizalisha katika mashamba yetu ili kuwa na mbegu ya kutosha lakini pia tunazijaribu ili kupata mbegu zenye ubora,” Alifafanua 


“Kingine kunachokifanya katika benki yetu ya  mbegu ni kusambaza kwasababu banki hii sio makumbusho useme watu watakuja kuangalia na kuondoka, mbegu lazima itumike kwaajili ya uzalishaji kwahiyo tunasambaza mbegu kupitia miradi ya kimaendeleo ambayo inawafanya wakulima kuweza kuzifikia mbegu hizi na kuweza kuzitumia katika bustani za nyumbani, za Shule na maeneo mengine,” Alisema.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI