Header Ads Widget

VIJANA WAASWA KUCHANGAMKIA FURSA YA KILIMO CHA KAHAWA


Aliyesimama katikati ya vitalu vya kahawa  ni Afisa Maendeleo zao la kahawa Kanda ya Magharibi Jasson Michael kutoka bodi ya kahawa Tanzania

Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu (wa pili kushoto)na Viongozi wa CCM Halmashauri ya Tanganyika wakimkabidhi mkulima wa zao la kahawa mche wa kahawa Bora katika Kijiji cha Mwese Halmashauri ya Tanganyika Mkoani Katavi

Na Diana Rubanguka,  Katavi

Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika wametakiwa kuchangamkia fursa ya kilimo cha zao la kahawa lengo likiwa  kujiinua kiuchumi,kuongeza uzalishaji wa zao hilo pamoja na pato la taifa.


Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa miche bora ya kahawa katika vitalu sita vilivyopo kijiji cha Mwese Halmashauri ya Tanganyika Mkoani Katavi, Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu ametoa rai hiyo baada ya kuona idadi kubwa ya wakulima wa zao hilo la kahawa katika Kijiji hicho ni wazee.


Amewataka vijana badala ya kucheza pool table,kukaa vijiweni walime zao la kahawa kwani linatija na ukanda huo unaardhi inayokubali kilimo cha mazao ya aina yoyote.


 Afisa Maendeleo zao la kahawa Kanda ya Magharibi Jasson Michael kutoka bodi ya kahawa Tanzania amesema mpango mkakati wa  bodi ya kahawa ni kuongeza uzalishaji wa zao hilo kutoka tani  82,000 za sasa hadi kufikia tani 300,000 kitaifa.


Amesema ilikufikia lengo hilo miche ya kahawa Bora zaidi ya laki sita imepandwa katika Halmashauri ya Tanganyika kupitia bodi ya kahawa na ndio imegawiwa kwa wakulima wa kahawa maeno ya Lugonesi na mwese kwa ajili ya uzalishaji.


Jasson amesema uzalishaji wa miche hiyo umegharimu shilingi Milioni 75 na kuwataka wakulima waliogawiwa miche hiyo kwenda kuipanda na kuitunza kwani ni zao lenye tija na kuwahamasisha wakulima wengine kulima  zao hilo la kahawa.


Mwenyekiti wa Chama  cha Mapinduzi (CCM) Halmashauri ya Tanganyika Yasin Kiberiti amewataka wakulima waliogawiwa miche ya kahawa bora wakaipande katika mashamba yao na sio kuiweka chini ya miti na kuoza.


Kiberiti amesisitiza vijana kujikita katika kilimo cha kahawa  na kuachana na mawazo ya kuwa zao hilo linakaa shambani   kwa muda mrefu na fedha yake haipatikani kwa uharaka.


Miongoni mwa wakulima wa zao la kahawa katika Kijiji cha Mwese Inviocaviti Shoo ameishukuru serikali kupitia bodi ya kahawa kuwapatiwa mbegu bora ya kahawa kwani wameanza kilimo hicho  miaka mingi na mpaka sasa bado wanalima na ndio uti wa mgongo wa maisha yao na urithi walioachiwa na wazazi wao.


Shoo amesema kilimo cha kahawa kimemsaidia kusomesha watoto wake pamoja na kuinua kipato cha familia yake kwa kupata mahitaji mbalimbali ya nyumbani.


Nae Venera  Kanizius mkulima na mzalishaji wa miche ya kahawa ameishukuru Bodi ya kahawa kwa kusimamia uzalishaji wa zao la kahawa katika Kijiji chao na kuwapatia miche Bora kwa ajili ya uzalishaji na kuahidi hatokiacha kilimo cha kahawa japo umri umemuacha.


"napata faida nzuri kwa kuuza miche ya kahawa ninayoizalisha  kila mche mmoja nauza shilingi 150 na hapa nyumbani kwangu nimezalisha miche elfu arobaini ukiangalia napata faida  ambayo inanisaidia kujikimu kimaisha Mimi pamoja na familia yangu"alieleza Venera.


Afisa ugani Kijiji cha Mwese Lawrence Elias ameahidi kusimamia wakulima wa zao la kahawa na kuhakikisha uzalishaji unaongezeka kutoka tani 5 hadi tani 100 ifikapo mwaka 2028 katika Kijiji hicho.



Baadhi ya wakulima wa zao la kahawa katika Kijiji cha Mwese Halmashauri ya Tanganyika Mkoani Katavi wakiwa na miche ya kahawa Bora baada ya kugawiwa kwenda kupanda

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI