NA WILLIUM PAUL, ROMBO.
MBUNGE wa Jimbo la Rombo ambaye pia ni Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa maandalizi yote ya mashindano ya mbio zijulikanazo kama Rombo marathoni na Ndafu festival yameshakamilika na kuwataka wananchi kuanza kujitokeza kujisajili.
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri huyo alisema kuwa mbio hizo zitakazofanyika Disemba 23 mwaka huu Tarakea wilayani Rombo kupitia msitu wa Rongai zinafanyika kwa mara ya pili ambapo kwa sasa wanategemea kuwa na washiriki 1000.
Alisema kuwa, fedha zitakazopatika katika mbio hizo zitatumika kukamilisha kampeni ya ujenzi wa vyoo bora na vya kisasa katika shule za msingi na Sekondari jimbo la Rombo pamoja na upanuzi wa hospitali ya Huruma ili iwe ya kiwango cha mkoa.
Mkenda alidai kuwa, zipo baadhi ya changamoto ambazo zilionekana katika katika mbio za mwaka jana ambapo kwa sasa zimeshafanyiwa kazi ili kuhakikisha washiriki wote wanafurahia ikiwemo ubadilishaji wa njia ya kukimbilia.
0 Comments