NA MATUKIO DAIMA APP,ZANZIBAR
Rais Wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewataka watafiti nchini kuhakikisha wanafanya tafiti zenye tija ambazo zitaishauri serikali namna bora ya kuendelea kuboresha mazingira ya biashara pamoja na kutoa ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili Wafanyabiashara na Wananchi.
Akisoma hotuba ya Rais Dkt. Mwinyi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla katika ufunguzi wa Kongamano la Pili la Kimataifa la Usimamizi wa Biashara na Maendeleo ya Uchumi Hotel Verde mjini Unguja.
Alisema Serikali kwa kushirikiana wataalamu itaweza kuja na suluhisho ndelevu kwa changamoto zilizopo na kuepusha kuendelea kutumia fatiti za nje ambazo nyingi sio sahihi kwa mazingira, teknolojia na historia ya nchi.
Aidha, aliwataka wataalamu na watafiti kutumia Kongamano hilo kubadilishana uzoefu na watafiti wa nje ili kuchota uzoefu na ujuzi kwa watafiti wa nje na kujikita katika kuhuisha tafiti zenu ili ziendene na mazingira.
Sambamba na hayo, alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zitaendelea kuwekeza katika kujenga mazingira wezeshi ili kujenga uchumi imara unaojumuisha sekta rasmi na zisizo rasmi.
Hata hivyo, alisema hatua hiyo imewezesha kuwa na uwekezaji mkubwa katika miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Barabara, Reli, Madaraja ya kisasa, Bandari na Viwanja vya Ndege.
Waziri ya Fedha na Mipango, Dkt. Saada Mkuya Salum, alisema, kongamano hilo litasaidia katika kutoa elimu ya namna ya kuendeleza uchumi endelevu na kuleta tija na kuweka mfumo mzuri wa biashara.
Alisema bila ya usimamizi mzuri wa fedha hakutakuwa na uchumi endelevu sambamba na kuchochea masuala ya maendeleo.
Naye, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya uhasibu Tanzania (TIA) Prof William Amos Pallangyo, alisema, Taasisi yao imejikita kutoa elimu yenye ushindani katika biashara, kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaamamu katika maeneo ya uhasibu, ununuzi na ugavi.
Aidha, alisema maeneo mengine ya biashara ikiwemo uongozi wa biashara, usimamizi wa rasilimali watu, masoko na uhusiano wa umma na usimamizi wa miradi.
Hivyo, alisema TIA itaendelea kusogeza elimu karibu na watanzania katika maeneo mbalimbali nchini na kusema kwa sasa TIA ina kampasi saba yenye jumla ya wanachuo wapatao 26,000.
0 Comments