Na Thobias Mwanakatwe,Singida
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imezitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD) zisiwe kikwazo cha kukwamisha miradi mbalimbali ikiwamo ya umeme.
Kufuatia hali hiyo PAC imeiagiza Serikali kuzisimamia taasisi hizo ili ziwe zinafanya kazi kama timu kwani miradi inapochelewa kwasababu ya taasisi hizo kunasababisha ongezeko kubwa la gharama za miradi.
Wabunge wa kamati hiyo wametoa agizo hilo juzi baada ya kutembelea mradi wa usafirishaji umeme unaojulikana Backborn Transmission Invtestment Project (BTIP) ambao unalenga kuziunganisha kwa nishati ya umeme nchi za Tanzania,Kenya,Ethiopia na Zambia.
Wabunge wa kamati hiyo walitembelea mradi huo kujiridhisha maendeleo yamefikia wapi kwasababu mwaka jana kujitokeza changanoto kadhaa ikiwamo ya wafadhiri waliokuwa wameahulidi kutoa fedha walijitoa na hivyo kuathiri mradi na wakati huo serikali ilikuwa ikwishatoa zaidi ya Dola za Marekani milioni 400 kujenga miundombinu.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Japhet Hasunga,alisema katika utekelezaji wa mradi huo TANROAD wamepandisha gharama sana za usafirishaji wa mizigo wakati tayari mkataba ulishasainiwa jambo ambalo linasababisha kuongezeka kwa gharama za mradi na hivyo kuwapa mzigo watanzania.
Alisema kwa upande wa TRA, vifaa ambavyo havitakiwi kulipiwa kodi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi huo serikali iwe inafuatilia na wanatekeleza kwa wakati kwani kumekuwa na tatizo la kuchelewesha kutoa vibali na GN na kusababisha mkandarasi kusimama kuanza kazi jambo ambalo linawaumiza na kuwaingiza hasara Watanzania.
Hasunga alisema kamati yake imejifunza kwamba miradi mingi inayotekelezwa hapa nchini inachukua muda mrefu sana kukamilika kwa wakati kuliko ule muda unaokuwa umewekwa kwenye mikataba kwasababu wakati mwingine serikali inachelewa kutoa fedha za kianzio (advance payment) na hivyo kusababisha mradi kuchelewa na gharama za mradi kuongezeka.
"Tunataka mfano ujenzi wa 'substation' ya Shinyanga ambayo mumetweleza mtaujenga kwa miaka mawili,tunataka ndani ya muda huo uwe umekamilika ikizidi hapo gharama zitaongezema,kwa hiyo serikali ihakikishe inatoa fedha mapema kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo," alisema.
Naye Mbunge wa jimbo la Masasi Geofrey Mwambe, alisema inashangaza kama nchi TANROAD inaweza kuongeza tozo mbalimbali ambazo zinakwamisha miradi ya serikali kitu ambacho hakiingii akilini na TRA inatoza kodi ya VAT kwa vifaa ambavyo inatakiwa visamehewe kwenye miradi ambayo ni ya serikali .
"Kwa sheria za usimamizi wa kodi yapo maeneo ambayo Waziri wa Fedha ana mamlaka ya kuondoa lakini haifanyika,nafikiri kuna haja ya kuweka 'blankents provisions' za kwenye sheria ili miradi ya serikali isisumbuke kuhangaika kutafuta misamaha maana mambo haya yanachelewesha miradi na kujikuta tunaliwa fedha nyingi sababu mradi unachelewa kukamilika,"alisema.
Mwambe alisema changamoto kama hizi zinapojitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi zinasababisha ongezeko la gharama mambo hayo kujitokeza mara kwa mara ni aibu na sawa na kwamba sheria zetu tunazozitunga zinatuadhibu wenyewe.
Aidha,Mwambe alihoji suala la gharama za umeme utakaopatikana baada ya utekelezaji wa mradi huo kwani serikali kamwe haijawahi kufanikiwa inapoahidi upatikanaji wa umeme kwa gharama nafuu.
"Mwaka 2004 Mtwara wakati inatangazwa upatikanaji wa gesi asilia tuliahidiwa kwamba sasa uzalishaji wa umeme utakuwa mkubwa na gharama zitapungua kitu ambacho hakijawahi kutekelezwa hadi sasa," alisema.
Naye Mratibu wa Mradi wa Kenya-Tanzania Power Interconnector Project (KTPIP),Mhandisi Peter Kidadye, alisema wakati wa utekelezaji wa mradi huo wamejifunza kutokana na changamoto zilizojitokeza kwenye suala la kodi na kusababisha kulipa fidia wakandarasi kutokana na kuchelewa kuanza kwa mradi kwasababu mgogoro wa kodi.
Alisema tatizo hilo la utozaji wa kodi lilijitokeza kwa Tanzania pekee wakati nchi ya Kenya wao hakukuwa na tatizo kutokana na utaratibu mzuri waliouweka kwenye utekelezaji wa miradi inayojengwa na serikali na kuwaomba wabunge miradi mipya itakapoanza kutekelezwa wadau wote mfano TRA,TANROAD washirikishwe kwa karibu ili kusiwe na mivutano.
"Mfano mdogo kwenye msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa mizigo ambayo inaingizwa toka nje kwa ajili ya kutekeleza mradi huu wa KTPIP tulipoteza miezi 11 kwasababu TRA haikukubaliana kutoa mizigo ili mradi uendelee kujengwa wakati majadiliano ya kulipa kodi yakiendelea, haya mambo ni kama tulikuwa tunajipiga risasi wenyewe" alisema.
Kidadye alisema pamoja na kwamba suala hili ni la sera na lina sheria lakini kuna umuhimu wa kuliangalia na kulipatia ufumbuzi maana nchi kama Kenya haikuathirika kama ilivyokuwa kwa Tanzania kwasababu wao waliangalia suala hilo kwa maslahi mapana ya taifa lao.
Awali Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco, Mhandisi Dk.Cosmas Masawe,aliwaeleza wabunge hao kwamba TRA na TANROAD wamekuwa kikwazo katika utekelezaji wa miradi ya umeme kutokana na kuidai Tanesco gharama nyingi na kusababisha kuchelewesha mradi.
Dk.Masawe alitaka sheria kinzani zirekebishwe ili zisaidie kuendeleza niradi kwa gharama nafuu na pia wabunge wasaidie malipo ya awali kwa mkandarasi yafanyike mapema kwa ajili ya kujenga kituo cha kusafirisha umeme Shinyanga.
0 Comments