NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MVUA zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini zimesababisha madhara makubwa katika halmashauri ya Moshi mkoani Kilimanjaro huku baadhi ya vijiji vikigeuka kuwa visiwa baada ya kuzungukwa na maji hali inayopelekea wananchi kukosa makazi.
Hali hiyo imepelekea Baraza la Madiwani katika halmashauri hiyo kuombe kitengo cha Maafa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kuchukua hatua za haraka kuwanusuru wananchi hao kabla madhara hayajawa makubwa.
Akizungumza katika Baraza hilo jana, Diwani wa kata ya Arusha chini, Leonard Waziri alisema kuwa, katika kata hiyo vijiji vya Chemchem, Mikocheni vipo katika hali mbaya zaidi ambapo baadhi ya makazi ya watu yakiwa yamesomwa na maji.
"Kata ya Arusha chini hali ni mbaya sana vipo vijiji vimegeuka kuwa kisiwa hakuna barabara inayoingia wala kutoka isipochukuliwa hatua za haraka kuwaokoa wale wananchi madhara yatakayotokea ni makubwa sasa hatupaswi kusubiria hilo litokee" Alisema Waziri.
Diwani huyo aliendelea kudai kuwa, kwa sasa wamelazimika kufunga baadhi ya shule katika kata hiyo kutokana na walimu pamoja na wanafunzi kushindwa kufika shule kutokana na maji kutapakaa kila mahali.
Alisema kuwa, mvua hizo pia zimepelekea uharibifu mkubwa wa mazao na vyakula ambapo wananchi kwa sasa wanahitaji msaada wa vyakula pamoja na makazi mavazi.
Waziri alisema kuwa, hatua zisipochukuliwa haraka upo uwezekano mkubwa wa kuibuka magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu kutokana na wananchi kunywa maji yasiyo safi na salama.
Kwa upande wake, Diwani wa Mabogini, Dkt. Bibiana Masawe alisema kuwa, katika kata yake kwa sasa hakuna mawasiliano ya barabara na kuiomba Tarura kuchukua hatua za haraka kurejesha mawasiliano.
Dkt. Bibiana alisema kuwa, kwa sasa wananchi wanalazimika kutembea kwa miguu umbali mrefu ili kupata usafiri Getifonga ambapo ni hatari kwa mama wajawazito pamoja na wagonjwa.
Akitoa taarifa za madhara yaliyosababishwa na Mvua hizo, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Shadrack Mhagama alisema kuwa jumla ya kata sita katika halmashauri hiyo zimeathirika na mvua zinazoendelea kunyesha.
Mhagama alizitaja kata hizo kuwa ni Old Moshi magharibi, Kahe magharibi, Uru kusini, Kilema kusini, Arusha chini na Mabogini.
Alisema kuwa, athari zilizotokea ni vifo vya watu watatu, majeruhi, upotevu wa mifugo, uharibifu wa mazao, maji kufurika na kutapakaa kwenye makazi ya watu na uharibifu wa miundombinu.
Alisema kuwa, halmashauri hiyo inaendelea kufanya tathimini ya kina ya uharibifu wa mazao inaendelea pamoja na kusambaza dawa za kutibu maji pamoja na kupuliza dawa ya kuzuia kipindupindu na kugawa neti za kuzuia mbu.
Mwisho.










0 Comments