NA HAMIDA RAMADHANI, MATUKIO DAIMA AAP DODOMA
WAZIRI wa Fedha Dk. Mwigulu Nchemba amesema kasi ya ukuaji wa uchumi kwa Taifa imeendelea kukua huku ikikadiliwa kufikia asilimia 6.2 muda mfupi ujao.
Amesema kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFM) uchumi wa Tanzania umeendelea kukua kwa wastani wa asilimia 5.2 licha ya kuwepo kwa changamoto za UVIKO, mabadiliko ya tabia nchi, vita vya Urusi na Ukraine na vita ya Israel na Palestina.
Dk. Mwigulu aliyasema hayo jijini hapa katika hotuba yake iliyosomwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Jenifa Omolo, aliyemuwakilisha katika mahafali ya 37 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP).
“Kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia na IFM uchumi wetu umeendelea kukua kwa wastani wa asilimia 5.2 pamoja na kuwepo kwa changamoto mbalimbali za UVIKO, mabadiliko ya tabia nchi, vita vya Urusi na Ukraine na sasa vita ya Israel na Palestina. Inakadiriwa kuwa muda mfupi ujao uchumi wetu utakuwa kwa alimia 6.2,”alisema.
Akizungumzia kuhusu mikopo ya elimu ya juu Jenifa alisema, serikali imeendelea kuongeza bajeti ya mikopo ili kuwawezesha vijana wengi kunufaika.
Alisema katika mwaka huu wa fedha 2023/24 serikali imetenga sh. bilioni 731 ikilinganishwa na sh. bilioni 570 zilizotengwa mwaka wa fedha uliopita.
Jenifa alisema lengo la kuongeza idadi ya wanufaika wa mikopo ni kuongeza idadi ya wataalamu katika fani hizi za kipaumbele ilikutekeleza maazimio ya Afrika kuhusu rasilimali watu.
“Katika mwaka huu wa masomo serikali imetenga sh. bilioni 48 kwa ajili ya kuwakopesha wanafunzi 8,000 wa ngazi ya stashahada katika fani za afya na sayansi shirikishi, elimu ya masomo ya fizikia, hisabati, Kemia na na masomo ya amali,”alisema
Aliongeza kuwa :”wanafunzi wengine watakaonufaika na mikopo hiyo ni wa usafiri na usafirishaji, uhandisi wa nishati, madini na sayansi ya ardhi na kilimo na mifugo.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo cha IRDP Profesa. Hozen Mayaya, alisema katika mwaka wa masomo ulioisha chuo hicho kiliendesha mafunzo ya muda mrefu katika programu 26 katika fani mbalimbali za mipango ya maendeleo kuanzia ngazi ya astashahada hadi shahada ya uzamili
Alisema idadi ya wahitimu katika chuo hicho imeendelea kuongezeka kila mwaka.
“Mbele yako katika mahafali haya kwa mwaka 2022/23 ni wahitimu mahiri 6,362 ambapo kati yao wanaume ni 2,783 na wanawake ni 3,579 ikiwa ni ongezeko la wahitimu 137 ukilinganisha na wahitimu 6,225 kwa mwaka wa masomo 2021/22,”alisema.
Profesa. Mayaya alimpongeza, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo serikali yake ya Awamu ya Sita imeendelea kukiwezesha chuo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Alifafanua kuwa hatua hiyo ya serikali imewezesha chuo kuendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia hususani katika miundombinu na rasilimaliwatu.
“Utashi huu wa serikali umetupatia sisi wanajumuiya ya chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini tuna deni kubwa la kulilipa. Tunakuahidi kuwa tutalilipa deni hili kwa uaminifu mkubwa kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii, maarifa na weledi mkubwa huku tukiweka mbele maslahi ya taifa letu,”alisema
0 Comments