Header Ads Widget

JUMUIYA YA WAFANYABIASHARA TANZANIA (JWT) YAHAMASISHA WAFANYABIASHARA KULIPA KODI KWA HIYARI

JUMUIYA ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) imesema itaendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara nchini ili waunge mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kuleta maendeleo kwa wananchi kwa kulipa kodi kwa hiyari.


Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) Taifa Hamis Livembe alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara wa Wilaya ya Kibaha wakati wa ziara yake kutembelea Mkoa wa Pwani.


Livembe amesema kuwa kila upande una wajibu kwa mwenzake ambapo serikali inaweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na kwa wafanyabiashara kazi yao ni kulipa kodi ambapo wataendelea kutoa elimu ya ulipaji kodi kwa kufuata sheria.


"Naombeni wafanyabiashara mlipe kodi kwa hiyari kwani serikali imeweka mazingira mazuri ya sisi kufanya biashara na hata kama kuna changamoto imeacha milango wazi kwa ajili ya majadiliano kama kuna kero kuhusiana na kodi,"amesema Livembe.


Naye Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Rashid Mchatta alisema kuwa Jumuiya hiyo inafanya kazi kubwa ya kizalendo kwani nchi inapokusanya vizuri mapato yanarudi kwa wananchi kwa kutoa huduma kwa ufanisi hivyo kulipa kodi ni muhimu na kama kuna changamoto watashirikiana na wafanyabiashara kuzitatua kwa pamoja ili mazingira ya biashara yawe rafiki.


Kwa upande wake mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara (JWT) Mkoa wa Pwani Abdala Ndauka amesema kuwa wanaishukuru serikali kwa kutatua baadhi ya changamoto za wafanyabiashara.


Moja ya wafanyabiashara ambaye ni mwanachama wa Jumuiya hiyo Mkoani humo Hassan Msemo amesema kuwa moja ya changamoto wanazozipata ni baadhi ya viwanda kutokuwa na stoo za kuuzia bidhaa wanazozizalisha ambapo nyingi ziko Jijini Dar es Salaam hivyo kuwagharimu kuzifuata.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI