Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA
TATIZO la uhaba wa mbolea ya kutosha kwa wakulima nchini litakwisha ifikapo 2024 kufuatia mwekezaji wa kampuni ya Intracom Fertilizers Limited kuanza ujenzi wa viwanda vitano vya kuzalisha mbolea vinavyojengwa mkoani Dodoma vitakavyokuwa na uwezo wa kuzalisha tani milioni moja kwa mwaka.
Uzalishaji huo utakuwa ni zaidi tani 300,000 ya mahitaji ya mbolea tani 700,000 zinazotumika hapa nchini.
Meneja wa Maendeleo ya Biashara na Masoko wa kampuni ya Intracom Fertilizers Limited, Dk.Keneth Masuki, alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa hafla ya uzinduzi wa ghala la kuhifadhia mbolea aina ya Fomi inayozalishwa na kampuni hiyo ambao ulifanywa na Mkuu wa Mkoa wa Singida,Peter Serukamba.
Alisema mpango wa awali wa mwekezaji ilikuwa ni kuwa na viwanda vitatu ambavyo kila kimoja kiwe na uwezo wa kuzalisha tani 200,000 kwa mwaka lakini kutokana na mahitaji makubwa ya mbolea nchini na changamoto zilizojitokeza,serikali ilimuomba apanue na kuongeza viwanda viwe vitano ambavyo vitazalisha tani milioni moja kwa mwaka.
"Kwa taarifa ya Mdhibiti Mkuu wa Mbolea Tanzania (TFRA) ni kwamba Tanzania tunatumia kati ya tani 600,000 hadi 700,000 kwa mwaka,hivyo viwanda hivi vikikamilika vitazalisha tani milioni moja vitalisha Tanzania nzima na kuwa na ziada ya mbolea ambayo itapelekwa kuuzwa katika soko la nje," alisema.
Masuki alisema tangu uzalishaji umeanza Disemba 2022 bado unaendelea kwa kiwanda kimoja na kwa sasa kiwanda namba mbili na tatu vipo katika hatua ya mwisho ya kukamilisha ufungaji wa mitambo na mwishoni mwa Novemba mwaka huu vitajaribiwa na ufikapo Disemba 2023 vinatarajia kuanza uzalishaji rasmi.
Aliongeza kuwa mitambo kwa ajili ya kiwanda namba 4 na 5 imeshafika 'site' na kinachosubiliwa ni wataalam kuanza kufunga mitambo hiyo ili ifikapo 2024 kuwe na jumla ya viwanda vitano ambavyo vitazalisha jumla ya tani milioni moja kila mwaka.
"Kuanzia mwakani (2024) mbolea itakuwa inapatikana kwa kiwango cha juu hapa nchini na hatakuwa na uhaba wowote, kwa sasa kiwanda kinazalisha mbolea za aina tatu ambazo ni Fomi Otesha,Fomi Kuzia na Fomi Nenepesha lakini aina mbili ndizo ambazo zinatumika sana na wananchi," alisema.
Masuki alisema katika kuhakikisha mbolea inawafikia wakulima kwa wakati kabla ya msimu wa kilimo kuanza, kwa kuanza kampuni imefungua magodauni ya kuhifadhia mbolea katika mikoa ya Mbeya,Njombe na Singida ambapo mpango ni kuwa na magodauni katika mikoa yote nchini," alisema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida,Peter Serukamba, alisema ujenzi wa viwanda hivyo vya mbolea ni mkombozi mkubwa wakulima ambao sasa watapata mbolea kwa wakati na pia wananchi zaidi ya 3000 watanufaika na ajira katika viwanda hivyo.
"Mbolea ya Fomi inatunza dhamani ya ardhi ambapo uhai wa ardhi utaendelea kama ikivyokuwa zamani na ukitumia Fomi mfululizo kwa miaka mitatu inawezekana mwaka wa nne usitumie mbolea kwasababu mbolea itakuwa ni nyingi na ardhi yako itaendelea kuwa kwenye thamani ya awali,mbolea nyingine zinaharibu thamani ya ardhi," alisema.
Serukamba alisema matumizi ya mbolea kwa wakulima yataongeza uzalishaji wa mazao na kuondoa umaskini kwa mkulima na itafanya Tanzania kuwa ghala la Afrika kwa chakula ambayo ni maono ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Alisema katika msimu wa kilimo mwaka huu wananchi waongeze uzalishaji na kupanua mashamba ili katika uzalishaji wa alizeti ambao Singida umefikia asilimia 50 ufike zaidi ya asilimia 70 na hivyo Singida iwe na uwezo wa kuzalisha mafuta ya alizeti ya kulisha nchi nzima.
"Wanasema Singida ni ya tatu kwa umaskini nataka tutoke huko tukianza kazi hii ya kilimo cha umwagiliaji nina uhakika Singida tutatoka huko kwenye namba tatu kwa umaskini," alisema.
Serukamba alisema ina miradi 92 inayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ambayo inaweza kumwagilia hektab160,820 ambazo ni zaidi ya ekari 400,000 na ni wa pili baada ya Mkoa wa Iringa kuwa na mradi mkubwa wa umwagiliaji unaojengwa kwa Sh.bilioni 32 katika Wilaya ya Mkalama.
Alisema serikali ya awamu ya sita ilipoingia madarakani bajeti ya kilimo ilikuwa ni Sh.bilioni 200 lakini mwaka huu bajeti katika Wizara ya Kilimo imeongezeka na kufikia zaidi ya Sh.bilioni 900.
"Bajeti hii ukiichakata utabaini fedha nyingi zimewekwa kwenye umwagiliaji,mbegu,utafiti na mbolea ya ruzuku, kwa hiyo rais Samia Suluhu Hassan ameanza safari ya kijani sababu ukiwekeza kwenye umwagiliaji uzalishaji utaongezeka mara tatu sababu watu watalima kwa misimu mitatu," alisema.
Aidha, Mkuu wa Mkoa alisisitiza kuwagiza Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanasimamia mbolea iwafikie wakulima kwa wakati ili kusiwe na visingizio .
0 Comments