NA MATUKIO DAIMA APP
BINTI wa miaka 19 Johari Twaha Mbuma mkazi wa Mawelewele kata ya Mwangata katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa mkoani Iringa anashikiliwa na jeshi la polisi mkoa wa Iringa kwa tuhuma za kumuua mtoto wake wa mkiezi 9 kwa kumtumbukiza kwenye ndoo ya maji chooni ili aende Dar es Salaam kuishi na mama yake mzazi .
Akizungumza katika mahojiano na Matukio Daima Media na uongozi wa serikali ya mtaa wa Mawelewela mjini Iringa Johari alisema kuwa maisha ambayo amekuwa akiishi Iringa yalikuwa magumu na baada ya kuwasiliana na mama yake alimtaka aende kuishi jijini Dar es Salaam ila sharti kubwa ni kwenda pekee yake bila mtoto .
" Mama alisema kwa kuwa nimekatisha masomo kutokana na ujauzito na nataka kwenda kuishi nae Dar es Salaam basi niende mwenyewe bila mtoto na kama nitakwenda na mtoto nisifikie nyumbani kwake ndio maana nikalazimika kumnyonga mtoto wangu na kumtupa kwenye ndoo ya maji ili nisafiri kwenda kuishi na mama Dar es Salaam" alisema Johari
Kuwa kabla ya kupata wazo la kuua mtoto huyo alifunga safari hadi eneo la Zizi la Ng'ombe kwa rafiki yake na iwapo angemkuta alipata kumtelekeza mtoto huyo kwa rafiki yake na yeye kusafiri kwenda Dar es Salaam ila baada ya kumkosa rafiki yake aliamua kumnyonga shingo mtoto huyo na kumtupa kwenye ndoo ya maji iliyokuwa ndani ya choo cha rafiki yake huyo kisha kutoweka .
Alisema mwanaume ambae alimpa ujauzito huo yupo Pawaga wilaya ya Iringa na kuwa toka mwanaume huyo ampe ujauzito hajawahi kuwasiliana tena wala hakuna huduma yoyote aliyokuwa akiituma kwa ajili ya kumsaidia mahitaji hivyo kupelekea kumpigia mama yake mzazi na kumuomba msamaha kwa kukatisha masomo ya sekondari.
Johari kwa sasa alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi wa kidato cha nne wanaotaraji kuhitimu masomo yao ya sekondari mwaka huu alisema anajutia uamuzi huo aliochukua ila hakuna na namna ya kufanya zaidi ya kufanya hivyo ili aende kuanza maisha mapya Dar es Salaam .
Chiku Mbuma ni bibi wa Johari akielezea tukio hilo alisema kuwa tukio la mjukuu wake huyo kuua mtoto lilitokea Jumapili Novemba 19 mwaka huu na kabla ya tukio hilo jumamosi ya Novemba 18 majira ya mchana walikutana na mjukuu wake huyo akiwa na mtoto mgongoni na hakumweleza chochote juu ya kuitwa na mama yake Dar es Salaam .
Alisema alishangazwa kuona anaitwa ofisi ya mwenyekiti wa serikali ya mtaa akielezwa juu ya kushikiliwa kwa Johari kutokana na tuhuma za kuua mtoto wake .
Faima Mohamed katibu wa umoja wa wanawake Tanzania (UWT) wilaya ya Iringa mjini alisema kuwa alijulishwa juzi mchana na diwani wa viti maalum kanda ya Mwangata Devotha Chaula juu ya tukkio la kukutwa kwa maiti ya mtoto huyo chooni ila mhusika wa tukio hilo hawakumkuta .
Alisema kutokana na mhusika wa mauwaji hayo kutojulikana waliendelea kufanya msako kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi vya kata na jeshi la polisi hadi jana asubuhi walipompata mhusika huyo .
Mohamed alisema UWT wilaya ya Iringa mjini imesikitishwa na unyama huo na kuwaomba wazazi kuwa jirani na mabinti zao hasa pale wanapopatwa na ujauzito ila kuwasimamia hadi wanapojifungua na kushirikiana kutunza watoto .
Diwani wa viti maalum kanda ya Mwangata Devotha Chaula alisema mtuhumiwa wa mauaji hayo alikamatwa jana asubuhi baada ya kurudi mtaani alipokuwa ameutupa mwili wa kichanga hicho kwa ajili ya kuchukua ili kwenda kutupa vichakani .
" Kwa kuwa toka jana tuliweka mkakati wa kumsaka binti aliyehusika na mauaji hayo wananchi na viongozi tulitawanyika kwenye mitaa mbali mbali kumtafuta mhusika wa mauaji hayo na ndipo asubuhi tulipomuona binti huyo akiwa eneo la tukio kutafuta mwili wa kichanga hicho tulimkamata na kumhoji bila kukataa alikubali kuwa ni yeye aliyefanya unyama huo"
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Mawele wele Obed Mtatifikolo alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kuwa tayari amekabidhiwa polisi kwa hatua zaidi za kisheria.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa (RPC) Allan Bukumbi alipotafutwa na mwandishi wa mwandishi wa Matukio Daima Media kwa njia ya simu jana majira ya saa 8;18 mchana hakupatikana hewani .
0 Comments