Header Ads Widget

WATOTO WA AWALI WATEMBEA KM 6 KUFUATA ELIMU NJOMBE MJINI



Afisa elimu msingi Halmashauri ya mji wa Njombe Mwalimu Shida Kiaramaba

Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Njombe  Erasto Mpete

Eneo la ujenzi wa Shule shikizi katika eneo la Block X mjini Njombe

Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP Njombe


Ili kukabiliana na changamoto ya watoto wadogo kutembea umbali wa takribani kilomita 6 hadi 8 toka eneo la block X mtaa wa Kambalage mjini Njombe kwenda kufuata elimu katika shule za msingi Kambalage Mpechi,Sabasaba na Mkombozi halmashauri ya mji wa Njombe imelazimika kutenga eneo lenye ukubwa wa ekari 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa shule shikizi.


Eneo hilo lililopo  Block X  limetajwa kwenda kuondoa changamoto hiyo kwa kuanza na madarasa matatu ya Awali,Darasa la Kwanza na la Pili madarasa ambayo yanakuwa na watoto wadogo ambao wamekuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu na kuhatarisha usalama wao.


Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Njombe Erasto Mpete ametembelea na kukagua eneo hilo ili kuweka mikakati thabiti ya kuanza ujenzi huo haraka iwezekanavyo.


Aidha Mpete amesema ni lazima wataalamu wawe mbele kuliko wananchi katika kuanza ujenzi huo kwani tayari kuna baadhi ya wadau wameshajitokeza kuchangia malighafi za kuanza ujenzi huo hivyo kama serikali inapaswa kuainisha ni wapi ujenzi utaanzia.


Ofisa elimu msingi halmashauri ya mji wa Njombe Mwalimu Shida Kiaramaba amesema kutokana na uwepo wa ukatili kwa watoto mkoani Njombe ipo haja ya kujenga shule hiyo ili kuwanusuru watoto wanaotembea umbali mrefu huku afisa ardhi wa halmashauri hiyo Amosy Luhamba akisema kutokana na udogo wa eneo hilo wanaweza kuanza kufikiria kujenga shule ya Ghorofa katika siku za usoni.


Hata hivyo Diwani wa kata ya Njombe Mjini Alatanga Nyagawa na Ofisa mtendaji kata ya Njombe Mjini Enosy Lupimo wamesema walichokuwa wanapigania kwanza ni kupata eneo huku wakiwaomba wadau mbalimbali wa elimu kuwashika mkono katika kufanikisha ujenzi wa shule hiyo.


Kwa upande wao wananchi na wazazi wa eneo la Block X akiwemo Yeremia Haule na Solanus Mhagama wamekiri kuwa watoto wao wanapata adha kubwa ya kupata elimu jambo linaloweza kudidimiza ndoto zao.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI