Header Ads Widget

AJALI YAUA VIONGOZI SITA (6) WA CCM MKOANI NJOMBE NA WENGINE KUJERUHIWA NJOMBE



Viongozi sita wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya Kata wakiwemo Viongozi watatu wa UWT kutoka Kata mbalimbali za Wilaya ya Makete Mkoani Njombe wamefariki kwa ajali ya gari wakati wakitoka kwenye mkutano wa Mlezi wa Chama hicho Mkoa wa Njombe Halima Mohamed Mamuya uliokuwa ukifanyika Wilayani humo.


Ajali hiyo imetokea Oktoba 13,2023 majira ya saa kumi na moja jioni katika kijiji cha Ndulamo baada ya gari Namba  T 733 BBP aina ya Toyota Hiece waliokuwa wamepanda kupinduka , Kamanda wa polisi mkoa wa Njombe John Imori amethibitisha kutokea kwa tukio hilo nakusema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi aliokuwa nao dereva nakushindwa kulimudu gari hilo.


Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe Juma Mfanga amesema majeruhi wengi wamevunjika viungo na wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Ikonda na wengine wakiendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Makete ambapo pia tayari Madaktari wengine kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe wamefika katika Hospitali hizo kuongeza nguvu.


Mjumbe wa Kamati kuu ya CCM Halima Mamuya ambaye pia ni Mlezi wa CCM Njombe ametoa pole kwa Familia na majeruhi ambapo amesema ajali hiyo imekuwa ni pigo kwake huku akiishukuru Serikali kwa hatua za haraka zinazochukuliwa kwa ajili ya matibabu “Waliofariki ni Viongozi wa Chama wawili,  Kiongozi wa Jumuiya ya Wazazi mmoja na Viongozi wa Jumuiya ya Wanawake watatu”


Naye Mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka kwa kufuatana na viongozi wa mkoa na Wilaya, wa chama cha Mapinduzi na Serikali leo wamefika kuwajulia hali majeruhi na kutoa pole kwao na kwa familia za waliopoteza maisha na kusema serikali ya mkoa itakuwa nao bega kwa bega kuhakikisha inagharamia majeruhi wanatibiwa na kupona, na marehemu wanazikwa kwa heshima zote.

“Tunajua kuna majeruhi ambao wamepata ajali hawana bima kwa hiyo Serikali ya Mkoa tunaelekeza matibabu yote yafanyike kwa usawa na gharama zile zije kwenye ofisi yetu ya Mkoa tuone namna ya kuweza kuzilipa" Mtaka


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS