Header Ads Widget

TAKWIMU ZA SENSA 2022 ZITUMIKE KUTEKELEZA MIPANGO YA MAENDELEO -RAIS UTPC


Na Editha Karlo,Kigoma


MATOKEO ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 yametakiwa kwenda kuisaidia jamii kujiletea maendeleo kwa kupanga mipango yao kutokana na takwimu sahihihi zinazopaswa kufikishwa na wanahabari weledi katika masuala ya takwimu.


Rais wa umoja wa vyama vya waandishi wa habari(UTPC)Deogratius Nsokolo ametoa wito huo wakati wa mafunzo ya siku mbili ya wanahabari zaidi ya 70 wa mikoa ya Kigoma,Rukwa na Katavi yaliyoandaliwa na ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)huku akisema endapo wanahabari wataelewa na kwenda kutumia takwimu hizo katika kazi zao itasaidia sana jamii kufahamu changamoto zao na namna ya kukabiliana nazo.


Nsokolo alisema kuwa matumizi ya matokeo ya sensa yatasaidia kuongeza uwazi,uwajibikaji kwa kuanzia ngazi ya Taifa hadi chini.

“Niipongeze ofisi ya Takwimu kwa kufanya ushirikishwaji kwa makundi yote  katika sensa ya mwaka 2022 hata mimi nilikuwa mjumbe wa kamati ya sensa ya Mkoa”alisema Nsokolo


Naye Kamisaa wa Sensa ya watu na makazi 2022 Tanzania Bara Anne Makinda spika mstaafu wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema wataendelea kutoa elimu kwenye makundi mbalimbali mpaka vijijini ili wananchi nao waweze kupanga na kutekeleza mambo yao.


Alisema wanahabari wanaweza kuisaidia vizuri jamii kujua ni kwa namna gani waweze kufuatilia mahitaji muhimu yanayopaswa kupelekwa kwao kutokana na takwimu kuonesha changamoto zote kila eneo nchini.


“Nyie ni kundi muhimu sana kupitia kalamu zenu mnaweza kuhamasisha jamii kutumia matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ili waweze kupanga na kutekeleza majukumu yao vizuri”alisema Makinda


Naye  Mtaalamu wa habari na mawasiliano toka ofisi ya Taifa ya Takwimu Said Ameir amesema mafunzo hayo kwa wanahabari yanapaswa kwenda kusaidia jamii kutekeleza shughuli za maendeleo kwa ushahidi wa kitakwimu.


Alisema matokeo ya sensa ya mwaka 2022 yatasaidia kuongeza maamuzi yenye ushahidi wa kitakwimu katika ngazi zote za utawala.


Kwa upande wao baadhi ya wanahabari kutoka mikoa ya Kigoma wameahidi kwenda kufanyakazi zao kwa weledi mkubwa kwa kutumia takwimu ambazo zitawapa mwanga wananchi kutambua hali ya maendeleo katika maeneo yao.


“Leo ni siku ya kwanza ya mafunzo yetu ila mafunzo haya ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 yamekuwa mazuri wawezeshaji wetu wametupitisha vizuri na sisi tutayafanyia kazi haya”alisema Glory Paschal mwandishi wa Radio ya Uvinza FM


Alisema watazitumia takwimu hizo kwa kufanya kazi kwa weledi ambapo wananchi watatambua hali ya maendeleo katika maeneo yao.


Sensa ya kwanza ya watu na makazi ilifanyika mwaka 1967 miaka 6 baada ya uhuru na mpaka sasa zimefanyika sensa 6 ikiwa ya mwisho imefanyika mwaka jana 2022.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS