Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MKUU wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye amesema kuwa kupooza kwa watoto au kupata ulemavu kutokana na ugonjwa wa polio hakuna mahusiano yoyote na masuala ya imani za kishirikina ambapo amewataka wananchi wote wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo ya ugonjwa huo.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Kigoma akitoa taarifa kuanza kwa zoezi la utoaji chanjo ya polio alisema kuwa ni makosa makubwa kuona mtoto anapata ulemavu au kupooza na jambo hilo kufanywa kuwa imani za kishirikiana jambo ambalo linaweza kuathiri watu watoto wengi zaidi.
Kutokana na hali hiyo Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa kwa sasa mkoa kigoma upo salama dhidi ya ugonjwa huo na kutaka wazazi kujitokeza kwa wingi katika zoezi la chanjo ya polio linaloanza Sept 21 hadi 24 kwa watoto chini ya miaka minane huku akieleza kuwa mkoa huo uko salama dhidi ya ugonjwa huo.
Awali Mkuu wa idara ya afya,ustawi wa jamii na Lishe kutoka wizara ya Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI), Gerlad Manase alisema kuwa katika awamu hii ambayo mikoa sita itahusika jumla ya watoto 884,478 watapata chanjo hiyo.
Manase alisema kuwa kutolewa kwa chanjo hiyo ni utekelezaji wa mpango wa dunia wa kutokomeza polio ambao imekuwa na athari kubwa kwa makuzi ya watoto kwa kusababisha watoto kupooza na kupata ulemavu.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa mkoa Kigoma Dk,Jesca Leba alisema kuwa mpango huo wa kutoa chanjo ya polio kwa watoto chini ya miaka minane utawahusu watoto wote ambao wapo mkoani Kigoma kwa sasa na zoezi la utoaji chanjo litafika maeneo yote hata yale magumu kukiwa na taarifa ya watu kuwepo huko.
0 Comments