Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kanda ya Nyanda za Juu Kusini imewaonya mawakala wa mbolea watakaojihusisha na udanganyifu wa aina yoyote kuhujumu zoezi la ruzuku ya mbolea kwa wakulima na kwamba hakuna atakayesalimika.
Onyo hilo linakuja kufuatia kuwapo kwa mawakala waliohujumu zoezi hilo katika msimu uliopita na kwamba wenye nia ya kufanya udanganyifu katika msimu huu pia wataangukiwa na mkono wa sheria ikiwemo kufutiwa leseni na kuburuzwa mahakamani.
Katika kikao na mawakala wa kuuza mbolea, vyama vya ushirika vya wakulima, maafisa kilimo na viongozi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea ,Meneja wa TFRA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini bwana Michael Sanga amesema tayari wana taarifa za kuwapo kwa baadhi ya mawakala ambao wameanza mchezo mchafu kwa wakulima.
Katika kikao hicho baadhi ya mawakala wa pembejeo akiwemo Absalum Magoma na Gaston Kaduma wameibua hoja mbalimbali na kuiomba serikali iwasaidie kwenye suala la madai yao huku wakiahidi kuwahudumia wakulima kwa weledi mkubwa.
Hata hivyo Mwenyekiti wa kamati ya pembejeo wilaya ya Njombe ambaye ni Mkuu wa Wilaya Mhe.Kissa Kasongwa ametoa maelekezo mbalimbali kwa wataalamu wa kilimo,Mawakala na TFRA ikiwemo kuongeza muda wa usajiri kwa wakulima pamoja na kuhakikisha wanazingatia bei elekezi ya mbolea kwenye kila kata.
Kwa upande wao baadhi ya wakulima toka kwenye vyama vya ushirika akiwemo Bwire William na Neema Kiwukila wamesema wataendelea kufuatialia hatua kwa hatua na kutoa taarifa pindi hujuma zozote zitakapojitokeza ili kuongeza tija kwenye kilimo.
Katika msimu huu wa Kilimo serikali imepeleka bei elekezi ya Mbolea kwenye kila kata hatua ambayo inapongezwa na wakulima.
0 Comments