Na WILLIUM PAUL, SIHA.
WATU kumi wamefariki dunia akiwamo Askari Polisi na mmoja kujeruhiwa baada ya gari la polisi kugongana na gari dogo la mizigo (Kirukuu), katika eneo la Datch kona wilayani Siha mkoa Kilimanjaro.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu alisema kuwa, ajali hiyo ilitokea jana ambapo wananchi tisa wakiwa kwenye gari la kirikuu wakielekea katika mnada wa mifugo wa Ngarenairobi wilayani huyo.
Babu alisema kuwa, chanzo cha ajali hiyo ni gari la Kirikuu kupasuka tairi na kukosa mwelekeo na kugongana na lori la polisi ambapo nalo lilikosa mwelekeo na kugonga mti.
“Kutokana na tukio hilo watu kumi wamefariki dunia pale pale kati ya hao tisa walikuwa kwenye gari ya kirikuu na dareva wake pamoja na dereva wa lori la polisi ambaye ni Askari polisi” alisema Babu.
Alisema kuwa, waliofariki katika ajili hiyo ni wanawake 6 pamoja na wanaume 4 akiwamo Askari Polisi.
Mkuu huyo wa mkoa alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wananchi kutambua kuwa magari aina ya kirikuu, pikapu na malori sio magari ya kubeba abiria bali ni magari ya mizigo hivyo ni marufuku wananchi kupakia magari hayo kama magari ya abiria.
“Tumekubaliana na Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro kuwa magari haya hayapakizi tena abiria lakini wapo baadhi ya madereva hawasikii wanapita Askari wanafika mbele wanapakiza abiria hata huyu Dereva wa Kirikuu alishapigwa faini kwa kosa la kupakiza abiria lakini amekuwa akirudia” alisema Babu.
Aidha Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa, majeruhi yupo katika hospitali ya wilaya ya Siha akipatiwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri huku miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya Kibong’oto kwa ajili ya taratibu za utambuzi.
Mwisho…









0 Comments