Na fatma Ally, Matukio DaimaApp , Dar
Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS Tanzania imesema imepata faida kutoka sh.bilioni 539 hadi sh.trilioni 1.5 sawa na asilimia 185, kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo, ambapo wamevuka lengo walilojiwekea awali tangu kuanzishwa kwa kampuni hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa UTT Amis, Simon Migangala katika kikao kazi na wahariri wa vyombo ya habar, ambapo amesema kuwa kiasi hicho cha faida ni kikubwa na hakijawahi kupatikana tangu kampuni hiyo ianzishwe ambapo lengo la awali la UTT AMIS ilikuwa ni kupata faida kutoka Sh.bilioni 290 hadi 485 kwa kipindi cha miaka mitano.
Amesema kuwa, awali uwekezaji katika mifuko hiyo ulikuwa na masharti magumu lakini sasa yamerahisishwa ili kuvutia zaidi wawekezaji.
Aidha, amesema UTT Amis wamefanikiwa kujitanua zaidi katika kuhakikisha kuwa wanafika kwenye maeneo mengi wanakopatikana wawekezaji hususan Mikoa mbalimbali ya Tanzania wilaya na vijiji na pia wana mawakala nchi nzima kupitia matawi ya benki ya CRDB ili wawekezaji wao wapate huduma.
"Awali ilimbidi mwekezaji wetu aende benki moja kwa moja ili kununua vipande, lakini kwasasa Mwekezaji anaweza kununua vipande kupitia njia zote za malipo za benki ya CRDB yaani Simubanking, CRDB App na Fahari Huduma pia kwa kutumia simu ya mkononi "amesema Mbaga.
Sambamba na hayo amesema kuwa lakini bado watanzania wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa elimu kuhusu umuhimu na faida za kutumia mifuko ya mitajia ya kifedha hususani kupitia UTT Amis katika kuwekeza fedha zao kwa malengo ya mda mfupi na mrefu.
Hata hivyo, amesema kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa watanzania kujitokeza kuwekeza katika mifuko iliyo chini ya kampuni hiyo, ila changamoto ambayo inawakabili ni uelewa mdogo wa watanzania kuhusu jinsi ya kuwekeza kwenye mifuko hiyo.
Ameongeza kuwa, watanzania wengi bado kipato chao ni kidogo hivyo wanahofia kuwekeza, katika mifuko hiyo kwa ajili ya malengo ya baadaye, hivyo kuishauri jamii kutumia mifuko hiyo kuwekeza hata kidogo walichonacho kwa faida ya baadae na kizazi kijacho.
Ameongeza kuwa, ili kuongeza idadi ya wawekezaji katika mifuko hiyo wataendelea kutoe elimu zaidi kwa wananchi ikiwamo kutumia vyombo vya habari na wanafunzi mashuleni ili kukuza uelewa kuhusu mifumo hiyo ya uwekezaji.
Hata hivyo, amesema UTT Amis imeendelea kuboresha uwekezaji wenye malengo ya muda mrefu na muda mfupi ili kuhakikisha kila mtanzania anapata fursa ya kuwekeza kwa manufaa ya kukuza kipato chake na taifa kwa ujumla.
"Kwa maisha ya sasa tunategemea fedha tofauti na miaka ya zamani ambapo wengi wetu tulikuwa tunarithishwa ardhi lakini sasa urithi wetu unategemea kwenye uwekezaji wa fedha hivyo niwahimize kuwekeza UTT AIMS kwani kila Mtanzania atajivunia,"amesema Mgangala.
Amesema Mfuko wa Jikimu ambao ndio maarufu hutoa mafao kila baada ya miezi mitatu, mfuko wa ukwasi ambao hauna hisa ambao unawekezaji baada ya muda unalipwa faida na hati fungani baada ya kuwekeza mwekezaji analipwa kila mwezi faida.
Aidha, amesema kwa sasa mfuko huo umekuwa kwa kasi ambapo hapo awali kulikuwa na akaunti za uwekezaji 500 kwa mwaka lakini mwaka huu zimefunguliwa akaunti 47,000 kutoka akaunti zilizofunguliwa mwaka jana 29,000. Pia una wawekezaji wanaofikia 300,000.
0 Comments