Header Ads Widget

SHUHUDIA UVUMBUZI WA KIATU CHENYE KIYOYOZI NA KICHEZA-MUZIKI


Na Simon Joshua - Matukio Daima App, Kisumu, Kenya.

Kijana mwenye umri wa miaka 21 kutoka kaunti ya Kisumu ametengeneza kiatu chenye uwezo wa kucheza muziki na kufanya masaji ya miguu.


Teddy Omondi, anayetoka Kajulu-Gita, alisema 'Project Cool Shoes', ni miongoni mwa ubunifu mwingi anaoufanya.

Alisema alisukumwa na hamu na kupenda teknolojia.


"Lengo langu lilikuwa ni kuja na uvumbuzi wa kipekee kwa ajili ya kuionesha dunia na watu wa Kenya," Amesema Omondi.


Anasema katika uvumbuzi wake, kila akipata wazo la kivumbuzi basi hulitia wazo hilo katika mchoro kabla hajaanza kulifanyia kazi.


Haikuwa rahisi kutokana na upungufu wa fedha, lakini alitumia viatu vyake mwenyewe kama modeli.


'T-TECH' (jina la kiatu) kina mfumo wa kucheza muziki na Bluetooth ambao unaweza kuunganishwa na simu janja au kicheza-muziki kitakachomrahisishia mtumiaji kuchagua aina ya muziki aupendao.


Kiatu pia kina mfumo wa kuzuia hitilafu ya umeme endapo nyaya zitapata hitilafu.


Kiatu kina kurunzi iliyowekwa mbele ya kiatu ambayo inaweza kutumika nyakati za usiku au mahali penye giza.


Kina sehemu mbili za ziada ambazo mtumiaji anaweza kuongeza idadi ya spika zingine kwa ajili ya kuongeza sauti.


Sehemu ya ndani ya kiatu kuna kiyoyozi kinachoweza kupunguza joto la kiatu katika halijoto na kuufanya mguu wa mtumiaji kuwa katika hali maridhawa.


Kiatu kina kitufe cha kubofya kwa ajili ya kufanya masaji.


"Hii sehemu ya Masaji ni muhimu kwa sababu imeunganishwa kwa kitetemeshi, ambayo husaidia wenye magonjwa ya miguu huku ikisaidia mzunguko mzuri wa damu," Alisema.


Omondi aliwaambia waandishi wa habari alitumia miezi mitatu kukamilisha 'Cool Shoes Project'.


Vifaa vingi alivyotumia viitoka katika duka la kukarabati simu kwa sababu hakuweza kupata fedha kwa ajili ya kupata vifaa vipya alivyohitaji.


Omondi ambaye ni mtoto wa mwisho katika familia ya watoto watatu anasema uvumbuzi unaweza kuwa fursa ya kujiajiri si tu kwa upande wake, bali hata kwa vijana wengine wa kiafrika katika nyakati ngumu za maisha.


"Hii ni fursa kwa vijana wenzangu wa kiafrika wenye vipaji, wasivikalie bali watumie uwezo wao kuionesha dunia."


Anasema hakuwa na bahati ya kujiunga na chuo kikuu kutokana na uhaba wa fedha ambao ulikwamisha masomo yake toka elimu ya sekondari ya juu.


"Nimelelewa na Mama tu na ninafurahi amekuwa mbaraka mkubwa sana kwa sapoti aliyonionesha kwa miaka yote hii." Alisema.


"Japo sikuweza kujiunga na chuo kikuu, alinihimiza siku zote kuendelea na uvumbuzi wangu kwani aliamini siku moja uvumbuzi huu utaniletea matunda ambayo yatakuwa faraja kwangu."


Omondi anasema ana miradi na vumbuzi nyingi ambazo zipo kwenye daftari ambapo moja ya miradi hiyo ni 'Spider Bag" ambalo litakuwa na na mfumo wa kibiometriki (fingerprint sensor) kwa ajili ya kufungua, sehemu ya kutunza vinywaji baridi na mfumo wa muziki kwa njia ya USB.


"Nimechora kila kitu, begi lina mfanano wa mdudu buibui na litakuwa na uwezo wa kutuma taarifa kwenye simu ya mmiliki endapo mtu mwingine atajaribu kulifungua." Alisema.


"Begi likigundua mmiliki yupo karibu, litatembea kwa kutumia miguu ya buibui kumfuata kama roboti."


Japokuwa anasema anaweza kufanya yote haya kama atapata mtu ambayo atamshika mkono au mwekezaji ambaye atavutiwa na uvumbuzi wake. 


"Kwa sasa, siwezi sema nitatengeneza viatu vingine kwa sababu sina pesa. Lakini nikipata mtu wa kunishika mkono au mwekezaji atakaevutiwa na uvumbuzi wangu, basi kila kitu kitaenda vizuri."

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI