Header Ads Widget

SERIKALI YASHAURIWA KUTOA MAFUNZO YA TEHAMA KWA WATENDAJI WAKE

 


NA THABIT MADAI,ZANZIBAR - MATUKIO DAIMA APP




KATIKA Kufikia Adhma ya Serikali ya kukuza Uchumi kwa Njia ya Digitali, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar SMZ imeshauriwa kuendesha Mafunzo mbalimbali kwa Watendaji wake kuhusu Tehama.



Wito huo umetolewa leo na Mwenyekiti wa Bodi wa Ushauri E- Goverment, Dk. Mzee Suleiman Mndewa, wakati akifunga kikao cha siku mbili cha kujadili rasimu ya sera ya serikali mtandao (E Government Policy) na mpango mkakati wa serikali mtandao (E Government Strategic Planning) ulioshirikisha wakurugenzi wa Mipango na IT kutoka serikalini kilichofanyika katika ukumbi wa Shekh Idrissa Abdul Wakili Kikwajuni.




Alisema pamoja na mkakati wa uchumi wa kidigitali, lakini bado juhudi za makusudi za kuwaelimisha wafanyakazi zinahitajika katika kutambua mfumo wa TEHAMA kwani baadhi yao hawana uelewa huo.




Aidha alisema Zanzibar asilimia 56 ya wafanyakazi wa serikali wa umma hawajui masuala ya TEHAMA hivyo ni vyema watendaji hao kujiendeleza kielimu ili kuiwezesha sera hiyo kufanyakazi na kufikia malengo yake.


 


“Imefika wakati sasa tujifunze na kuwafunza wenzetu kwani tukiwa hatutajifunza basi hatutaleta mabadiliko kwa taasisi zetu na kuyafikia malengo ya serikali yetu iliyojiwekea katika kufikia Zanzibar ya kidijitali,” alisema.




Hata hivyo, alisema katika taasisi nyingi hawajajiwekea sera zinazosimamia TEHAMA hivyo ni lazima mkuu IT katika taasisi kutengeneza sera ya taasisi ili kuona mambo ya TEHAMA yanafanyika vizuri.




“Unatakiwa uweke sera ambayo itasimamia taasisi yako katika masuala ya TEHAMA sio mtu anaingia tu anatumia kompyuta ambayo haina hata neno la siri ‘paswood’ hivyo nyinyi ni lazima kufuata miongozo inayotolewa na E- Government,” alisema.




Hivyo aliwataka wadau hao kuhakikisha mafunzo wanayafanyia kazi wanaporudi katika ofisi zao ili digitali ipate kuonekana na kuleta faida kwa nchi.


 


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa serikali Mtandao, Said Seif Said, aliwataka watendaji hao kushirikiana katika kufika azma ya kuwepo kwa sera hiyo ambayo itawezesha kutambuwa majukumu na kuyafanyia kazi kwa urahisi ili kwenda katika ulimwengu wa kidigitali.



Nao washiriki wa kikao hicho waliipongeza E- Government kwa kuwashirikisha katika utengenezaji wa sera na mikakati ya TEHAMA jambo ambalo limewawezesha kujifunza kwani litawasaidia kufanya kazi zao na kwenda na kasi ya maendeleo na tenkologia ilivyo kwa sasa.  



Ofisa Mkuu Mwantano Saleh Abdallah Mkuu wa kitengo cha TEHAMA Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Ofisa Mipango Mkuu Wizara ya Habari Vijana, Utamaduni na Michezo, Omar Juma Ali na Abubakar Victor ni Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA Wakala wa Usajili na Matukio ya Kijamii Zanzibar, walisema TEHAMA kwa sasa ndio inayoendesha dunia na bila ya kuwa na teknologia basi mambo ya serikali hayawezi kwenda vizuri.


Walisema sera na mikakati ndio maeneo muhimu ambayo yanasaidia katika kuifanya taasisi pale inapotoka na inapokwenda hivyo kuwepo kwa mafunzo hayo yamesaidia kuweza kujua Wakala wa serikali Mtandao anatakiwa kufanya kazi ili kuisaidia serikali kuimarisha huduma za kijamii.


“TEHAMA ndio inayotegemewa katika kuendesha serikali hivyo mfano huu ni mzuri ni vyema kwa taasisi nyengine kuiga mfano huu ili tupate kuwa na sera na mikakati ambayo itasaidia katika mambo ya TEHAMA,” alisema Mwantano.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI