NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA
Waziri wa katiba na sheria Dkt Damas Ndumbaro amesema kuwa wizara yake inategemea bodi ya taifa ya ushauri wa msaada wa kisheria itawashauri wanafanyaje ili kuweza kupata katiba mpya.
Dkt Ndumbaro aliyasema hayo wakati akizindua bodi hiyo, zoezi lililofanyika mkoani Arusha ambapo alisema kuwa watanzania wanahitaji katiba mpya hivyo wanategemea kupata ushauri utakawezesha kupata katiba ambayo haitamuacha mtu yoyote na itakayodumu kwa miaka mingi.
“ Nchi kwa sasa ina agenda kubwa mezani na agenda hiyo inaitwa katiba mpya,angalau kwenye hili wote tunakubaliana kwamba tunataka katiba mpya, tunaweza tukatofautiana tunaipataje hivyo sisi kama wizara tunategemea kwasababu suala la msaada wa kisheria ni suala la kikatiba na ni suala la haki za binadamu, bodi hii pia itatushauri tunafanyeje tuweze kuipata katiba mpya,” Alisema Dkt Ndumbaro.
“Tunafanyaje kupata katiba mpya, nzuri na yenye kuwafaa watanzania kwa miaka 100 ijayo kwani tuna mengi ya kujifumza kama watanzania kwakuwa toka tumepata uhuru hasa wa Tanzania bara hii katiba ni ya nne ndani ya miaka 60, kwanini tumekuwa na katiba nyingi ndani ya muda mfupi,” Alieleza.
Aliendelea kusema kuwa kutokana na kutungwa kwa katiba nyingi ndani ya muda mfupi kuna kitu hakipo sawa hivyo wanapoelekea kwenye katiba mpya ni lazima watafakari ili wawe na katiba ambayo itakaa muda mrefu, katiba ya wananchi ambapo wananchi watatoa maoni yao na watategemea bodi hiyo kuwashauri ili kufika huko, kuwa na katiba ambayo haitamuacha mtu nyuma.
“Moja ya kosa ambalo tunalifanya sana ni kuamini kuwa katiba ni mali ya wanasiasa, katiba sii mali ya wanasiasa bali ni mali ya kila mtu katika jamii husika wakimo wanasiasa kwahiyo mtushauri namna bora ambayo mwananchi mnyonge aliyeko Tandaimba, Misenyi, Jasini, Mbambabei anaweza kufikiwa, kushirikishwa na kutoa maoni yake juu ya hiyo katiba mpya,”Alisema.
Aliendelea kusema kwa kuwa suala la kisheria ni suala la haki za binadamu na wanajua haki za binadamu zinavuka mipaka kuna umuhimu wa kupata majukwaa ya kimataifa kwa bodi hiyo kuwashauri ni jinsi gani sula la msaada wa kisheria wanaweza kushirikisha watu wote ndani ya jumuiya ya Afrika Mashariki, SADIC,AU kwani kwakuwa na majukwaa hayo watapata fursa ya kujifunza kwa wenzao mazuri wanayopaswa kuyaiga na wao pia wapate fursa ya kujifunza.
Kwa upande wake Katibu mkuu wa wizara hiyo Mary Mkondo alisema kuwa weona mambo makubwa yaliyofanyikq kwa kipindi cha kwanza cha bodi hiyo hivyo wanatarajia makubwa zaidi yatafanyika kwa ushauri watakao utoa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa wanyonge, watanzania ambao hawawezi kupata haki zao wanasaidiwa kwa elimu na kwa taratibu za kisheria bure.
“Bado nchi yetu ni kubwa ina kilomita za mraba 905,000 kwa maana hiyo tukiangalia jukumu tulilonalo ni kubwa katika mikoa 26 lakini tunapaswa kushirikiana na upande wa Zanzibar ili watanzania wote waweze kupata haki katika vijiji vyote 12300 na kata 3900,” Alisemama Makondo.
Naye mmoja wa wajumbe wa bodi hiyo Faraja Nchimbi kutoka ofisi ya taifa ya mashtaka alisema kuwa wanashukuru kwa kuaminiwa na kurudi tena kwa awamu ya pili kuwa wajumbe wa bodi hiyo ambapo watatekeleza wajibu wao kwa weledi mkubwa na kuhakikisha watanzania wote wanapata msaada wa kisheria lakini pia haki zao.








0 Comments