Header Ads Widget

NJAA YAWAKIMBIZA WAKIMBIZI WA BURUNDI KIGOMA

 




Na Fadhili Abdallah,Kigoma



MWEZI mmoja baada ya Umoja wa Mataifa kupunguza kwa asilimia 30 bajeti ya kuhudumia wakimbizi nchini Tanzania hali hiyo imeonekana kuleta hali ngumu ya maisha kwa wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa kwenye kambi ya  Nduta wilayani Kibondo mkoani Kigoma ambao kwa hiari yao wameomba kupatiwa usafiri warundi nchini kukimbia adha hiyo.



Waandishi wa habari walishuhudia zoezi la uandikishaji linaloendelea kwenye kituo cha uandikishajo kambi ya wakimbizi Nduta ambapo idadi kubwa ya wakimbizi imejitokeza wakiomba kuandikishwa warudi nchini mwao.



Wakizungumza na waandishi wa habari kambini hapo Wakimbizi hao wamesema kuwa hali ya huduma kwa sasa ni mbaya hivyo hawawezi kuvumilia kuishi kambini hapo kama wafungwa hivyo ni bora taratibu zifanyike warudi nchini kwao Burundi.




Tofauti na wakimbizi wa kambi ya Nyarugusu wilaya ya Kasulu wanaotaka kwenda Ulaya wakimbizi hawa wa kambi ya Nduta wanataka kurudi nyumbani kukimbia hali hiyo.



Mmoja wa wakimbizi hao, Jean Claude Ntirushimana alisema kuwa mgao wa chakula umepunguzwa sana, huduma za matibabu na mambo mengi ambayo walikuwa wanapata kwa wingi ambavyo kwa sasa vina shida kupatikana.



Akizungumza na ujumbe wa serikali ya Burundi unaotembelea kambi za wakimbizi mkoani Kigoma Mkurugenzi idara ya wakimbizi ya wizara ya mambo ya ndani ya nchi, Sudi Mwakibasi alisema kuwa kupunguzwa kwa asilimia 30 ya bajeti ya kuhudumia wakimbizi ina athari kubwa kwa wakimbizi hao hivyo ni jambo jema kwa sasa kurudi.




Mwakibasi alisema kuwa kwa sasa mgao wa chakula kwa siku umepunguzwa kwa asilimia 50 na wakimbizi watakuwa wanapewa unga wa ngano badala ya  mahindi na huduma ya matibabu pia itaathiriwa kwa idadi kubwa ya wataalam kupunguzwa kazini.



Hata hivyo Mwakibasi alisema kuwa kwenye kambi ya wakimbizi ya Nduta wilayani Kibondo wakimbizi wengi wapo tayari kurudi akianisha uwepo wa wakimbizi 5199 waliojiandikisha mwezi Julai  kurudi nchini lakini UNHCR imewarudisha wakimbizi 1351 pekee huku juzi na jana wakijiandikisha wakimbizi 1096.



Akizungumzia Hali hiyo Katibu Mkuu wizara ya mambo ya ndani,  maendeleo ya jamii na usalama  wa Burundi,Calinie Mbashurimana alisema kuwa kupunguzwa kwa mgao wa chakula kwa asilimia 50 na kupunguzwa kwa huduma za afya kuna athari kubwa kwa afya na ustawi wa wakimbizi hao.




Kutokana na hilo kiongozi huyo ameitaka serikali ya Tanzania kusimamia mashirika ya Umoja wa Mataifa kuhakikisha huduma za kibinadamu zinatolewa kwa wakimbizi hao lakini kuweka taratibu na magari ya kutosha kuhakikisha idadi kubwa ya wakimbizi inarudishwa katika kipindi kifupi.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI