NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi ameendelea na ziara ya kutembelea Jimbo lake la Moshi Vijijini kwa kutembelea kijiji cha Mandaka Mnono kilichoko ukanda wa chini katika Kata ya Oldmoshi Magharibi.
Mbunge huyo alitembelea vikundi viwili vya wekeza (Shine na Baraka Groups), zahanati ya kijiji cha Mandaka Mnono, korongo la Manguvu na eneo kutakakojengwa Skimu ya Umwagiliaji ya Mandaka Mnono.
Aliambatana na na Katibu wa Wazazi Wilaya ya Moshi Vijijini Andrew Mwandu, Madiwani wa Viti Maalum kutoka Tarafa za Hai Mashariki na Kibosho, viongozi wa CCM Kata na Matawi kutoka Oldmoshi Magharibi na Watendaji wa idara mbalimbali toka Serikalini.
Mbunge huyo alijionea shughuli za kikundi cha Shine ambao wamejiunga kwa malengo ya kufuga mbuzi, kulima mpunga na kufanya biashara ndogo ndogo.
Wakisoma risala, walimweleza Mbunge kuwa wamepiga hatua kubwa, na wana nia ya kununua mashine ya kusaga, ila mtaji wao ni kidogo ambapo Mbunge aliahidi kuwachangia shilingi milioni moja.
Alipotembelea kikundi cha wekeza cha Baraka, Mbunge aliwapa moyo na kuwashauri waendelee kujipanga vizuri ili akirudi tena aangalie namna ya kuwasaidia kuongeza mtaji wao.
Alipotembelea zahanati ya Mandaka Mnono, Mbunge alielezwa kuwa wana changamoto ya maji ya kunywa na uhaba wa watumishi.
Mbunge na ujumbe wake walitembelea korongo la John Manguvu ambapo walipokea kero ya kutokuwepo kivuko cha kuunganisha vitongoji vya Saningo, Mnono Kati na Uswahilini.
Pia alitembelea bonde la Mandaka Mnono ambalo limepatiwa mradi wa Skimu ya Umwagiliaji ili kuendeleza kilimo cha mpunga.
Akiwa katika mkutano wa hadhara katika kitongoji cha Mnono Kati, Mbunge aliwaeleza wananchi juhudi kubwa zilizofanywa na serikali kuwaletea maendeleo katika sekta za elimu, kilimo, miundombinu ya barabara, umeme, maji na maendeleo ya jamii ambapo zaidi ya shilingi Bilioni 5.5 zimeshaelekezwa katika miradi hiyo ya maendeleo.
Katika mkutano huo, wananchi wakiwasilisha kero zao kwa Mbunge ambapo kero za ubovu wa barabara na maji safi ya kunywa ziliibuliwa na wananchi wengi waliopata nafasi ya kuongea.
"Hapa tunatatizo la kukosa kivuko katika korongo la kwa Saning'o hivi sasa hakuna kivuko na wakati wa mvua na mafuriko wanafunzi hushindwa kwenda shule jirani katika kata ya Mabogini pamoja na adha kubwa wanayopitia mama wajawazito kwenda zahanati ya Mnono" alisema mmoja wa wananchi.
Aidha wananchi hao waliomba kijiji cha Mandaka Mnono kuwa kata inayojitegemea huku pia wakilalamikia uharibifu wa makusudi unaofanywa na jamii ya wafugaji kwa kulisha mifugo katika mashamba ya wakulima.
Katika mkutano huo, kero ya uchakavu wa Shule ya msingi Saningo iliibuliwa pamoja na changamoto ya wakulima wa mpunga kulipia ada ya umwagiliaji ilipata ufafanuzi kutoka mtaalamu ya Tume ya Umwagiliaji ya Kanda ya kaskazini, na mwenyekiti wa Skimu ya umwagiliaji ya Mandaka Mnono.
Akijibu hoja za wananchi, Mbunge aliwaeleza wananchi kuwa kero zote amezipokea na atazifikisha Serikalini ili zipatiwe ufumbuzi.
Mwisho..
0 Comments