MWENYEKITI wa UWT Iringa Vijijini, Lenah Hongole amekuwa mgeni rasmi katika Kongamano kubwa la kupinga ukatili wa kijinsia lililo andaliwa na UWT Kata ya Mahuninga.
Kongamano hilo ambalo pia lilitumika pia kwa ajili ya kutoa elimu ya lishe liliandaliwa kwa ushirikiano na Madiwani wa Viti Maalum, Sophia Msekwa, Shani Msambusi pamoja na CCM kata ya Mahuninga.
Akizungumza kwenye Kongamano hilo, Hongole amesema Ilani ya CCM ya Mwaka 2020 inazungumzia pia masuala ya usawa wa kijinsia.
"Matokeo ya ukatili wa kijinsia ni umaskini, hatuwezi kuwa na Maendeleo kama ukatili wa kijinsia utaendelea. Kila mtu anajukumu la kukemea ukatili usiendelee," amesema Hongole.
Kulingana na Hongole, UWT Iringa vijijini itaendelea kufanya makongamano ya kupinga ukatili wa kijinsia ili jamii iwe salama na shughuli za kimaendeleo ziendelee kufanyika.
Aliwapongeza Mwenyekiti na Katibu wa UWT wa kata hiyo kwa maandalizi mazuri ya Kongamano yaliyoshirikisha makundi yote muhimu.
Pia alipongeza umoja na ushirikiano uliopo baina ya madiwani, Serikali na CCM kwenye kata hiyo.
0 Comments