Na Mbaruku Yusuph, Matukio Daima Muheza-Tanga.
JUMUIYA ya Wazazi Wilayani Muheza imetakiwa kutumia rasilimali zake ili ziweze kujikwamua kiuchumi na ziondokane na mfumo wa kujiendesha kwa kutegemea wahisani.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi mkoa wa Tanga Rajabu Abdurahman alipokuwa akikagua Shule ya Sekondari ya Mbaramo iliyopo kata ya Mbaramo Wilayani hapa inayomilikiwa na Jumuiya hiyo ambayo takriban miaka 6 imeshindwa kujiendesha.
Aidha alisema Jumuya hiyo ya wazazi ni miongoni mwa jumuiya zilizokuwa na rasilimali ya umiliki wa Shule hiyo ya Mbaramo sambamba na shamba kubwa na ni wakati wao wa kuanza kufikiria namna ya kutumia rasilimali hizo kwa maslahi ya jumuiya hiyo na chama kwa ujumla.
Alisema si jambo jema kuona jumuiya hizo zinakosa kipato huku zikiwa na rasilimali za kutosha zinazoweza kuwasaidia kujitegemea na ni wakati wa kujikosoa na kujisahihisha na kuonyesha fikra mpya ndani ya Jumuiya hizo.
"Ni bahati nzuri kwa jumuiya yetu hii kuwa na rasilimali ya shule na heka 52 za Shamba ijitegemee sasa mbali ya huo uwekezaji wanaotaka kuufanya wanaweza kulima shamba hilo na kujiongezea kipato"Alisema Rajabu.
Alisema katika ziara yake amekuwa mstari wa mbele kusimamia miradi ya maendeleo ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutoa maelekezo usimamizi huo unakwenda sambamba na kwenye miradi ya chama ili nao waweze kujitafakari pia.
Mwenyekiti huyo ambae yupo Wilayani Muheza ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa ziara yake ya Mkoa mzima wa Tanga kwa ajili ya kuangalia changamoto na kero zinazowakabili wananchi lakini pia kuangalia uhai wa chama sambamba na ukaguzi wa miradi ya maendeleo.
Mbali na hayo pia alizitaka jumuiya zote zitambue kuwa zinawajibu wa kuhakikisha zinajenga majengo ya kisasa ya ofisi zao na watambue kufanya hivyo ni kutii agizo la Chama cha Mapinduzi Taifa kupitia vikao vyake.
Rajabu ambae pia ni Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa alisema ili kufikia malengo hayo jumuiya hizo na Viongozi wa Chama ngazi ya Wilaya wanapaswa kushirikiana na Wabunge wao na wadau wamaendeleo ili waweze kufikia malengo hayo.
"Niwashauri ndugu zangu shirikianeni na Mbunge wenu na wadau mbalimbali na naamini kama mtalifanya jambo hili kwa ushirikiano mnaweza mkafanikiwa"Alisema Rajabu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya Muheza Khatib Bakari alisema tayari jumuiya hiyo imekwisaingia makubaliano na Tanga Development Forum kwa ajili kuwekeza katika swala la elimu katika Shule hiyo ya Sekondari ya Mbaramo.
Alisema muwekezaji huyo ambae ameingia makubaliano na Katibu Mkuu Taifa na atawekeza katika swala la elimu ya kuanzia awali hadi darasa la saba kwa muda wa miaka saba sambamba na urekebishaji wa miundombinu ya shule hiyo.
"Lengo na maudhui ni kuwekeza katika elimu na muwekezaji huyo amepewa muda wa miaka saba matumaini yetu atafanya vizuri na kufanya ufanisi mzuri katika sekta hiyo ya Elimu "Alisema Bakari.
Aidha alisema baada ya uchaguzi wa viongoI katika jumuiya hiyo na kuingia madarakani na kamati iliyopitishwa utekelezaji wa kwanza ni kuziweka mali za jumuiya vizuri na katika mpango sahihi wa matumizi.
"Mbali ya kuangalia uhai wa shule yetu lakini pia tuliona umuhimu wa kutafuta hati kabisa kabla ya mchakato wa uwekezaji kuanza ambapo matarajio utaanza mwakani 2024"Alisema Bakari.








0 Comments