Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima APP Dodoma
OFISI ya Taifa ya Mashtaka(DPP) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao imezindua mfumo wa kielektroniki wa kukusanya , kuchakata na kutunza Kumbukumbu za kesi jinai utakaoimarisha utendaji kazi.
Akizindua Mfumo huo Jana jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya utumishi na Utawala bora George Simbachawene amesema mfumo huo itasaidia kwa kiasi kikubwa utadhibiti makusanyo ya mapato ya Serikali.
Simbachawene amesema kupitia mfumo huo mpaka sasa zaidi ya kesi za jinai 17,411zimeshasajiliwa ambapo kati ya kesi hizo,7,361 zimeshafika mwisho na
kutolewa hukumu huku kesi 10,050 zipo Katika hatua mbalimbali za maaumzi.
Amesema,"kiukweli,haya ni mafanikio makubwa katika kuboresha utendaji kazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS),lakini pia ni mfano wa kuigwa na taasisi nyingine za umma zinazohusika na utoaji wa huduma kwa umma,"amesema
Amesema dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka
Mitano (2021/22 -2025/26), yote inatambua nafasi ya TEHAMA katika kufikia .
Naye Mkurungezi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba amesema malengo madhubuti ya mfumo huo ni kuhakikisha Taasisi zote za Umma zinaenda na wakati kwa kutumia TEHAMA.
Mhandisi Ndomba amesema kuwa mfumo huo umejengwa kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa taarifa
sahihi zinazohusu uendeshaji wa mashtaka na kusaidia katika uandaaji wa mipango ya ofisi na utoaji maamuzi mbalimbali pamoja na uandaaji wa taarifa zinazowasilishwa kwenye mamlaka nyingine.
Kwa Upande wake Naibu Waziri, Wizara ya Katiba na sheria Pauline Gekulu amesema mfumo huo ni muhimu hasa kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza matumizi yake Hali itakayo saidia kuimarisha na kurahisisha utoaji wa haki kwa wananchi.
Amesema katika kupitia dhamira hiyo huduma za serikali zitatolewa kidigitali na kumrahisishia mwananchi kupata huduma kwa haraka zaidi mahali walipo.
"Sote tunafahamu kuwa haki ni Suala muhimu sana na inapaswa kutolewa kwa wakati kwani haki iliyochelewa na sawa na haki iliyonyimwa hivyo Kupitia Mfumo wa TEHAMA tunataka kuhakikisha haki zote zinatolewa kwa wakati, "amesisitiza
Amesema, Sekta ya Sheria imejiwekea malengo thabiti katika kuboresha utendaji kazi wake kwa kutumia mifumo ya TEHAMA kupitia programu ya e-justice kuwezesha kupata taarifa za kesi mbalimbali zilizoshughulikiwa na hatua zilizofikia.
"Mfumo huu umeunganishwa Katika mfumo wa ubadilishanaji taarifa serikalini (GoVESB)na Hadi Sasa tayari unabadilishana taarifa za mifumo ya Jeshi la polisi pamoja na PCCB, "amefafanua.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Sylvester Mwakitalu amesema kupitia Mfumo huo utamsaidia kuharakisha kesi zilizokuwa zinalundikana na kusababisha wananchi kusubiri kwa muda mrefu na kupoteza imani na Serikali.
"Tunaishukuru Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa kutengeneza mfumo huu ambao kwa sasa naweza kufuatilia jinsi kesi zote zinavyoshughulikiwa na pale nitakapogundua kuwa kuna jalada limechelewa hapo hapo nauliza sababu za kuchelewa na linashughilikiwa kwa haraka,"amesema Mwakitalu
Ikumbukwe kuwa, utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao ni moja ya maeneo muhimu ya maboresho yaliyofanyika na yanayoendelea kutekelezwa katika Utumishi wa Umma, ambayo yamesaidia kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa Umma,hivyo, ujenzi wa mfumo huo ni muendelezo wa jitihada za Mamlaka za kuhakikisha Taasisi za Umma zinatumia vyema TEHAMA katika kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa Umma.







0 Comments