Header Ads Widget

WAZIRI AWESO AZIONYESHEA KIDOLE KAMATI ZA MAJI KULA KULA

Waziri wa maji Jumaa Aweso akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji cha Migongo wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma alipokuwa akizindua mradi wenye thamani ya shilingi Bilioni 1.2 ambao umekamilika na kuanza kutoa huduma.

Waziri wa maji Jumaa Aweso (kushoto) na Mbunge wa jimbo la Buhigwe Felix Kavejuru wakinywa maji kutoka bomba linalotoa maji  katika kijiji cha Migongo wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma alipokuwa akizindua mradi huo  wenye thamani ya shilingi Bilioni 1.2 ambao umekamilika na kuanza kutoa huduma.

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

WAZIRI wa maji Jumaa Aweso amezionya kamati za watumia maji kwenye miradi ya maji iliyokamilika na kuanza kutoa huduma kufuata miongozo iliyowekwa ya matumizi ya  fedha  zinazolipwa na wanachi ambapo ametoa maagizo kuchukuliwa hatua kwa viongozi wa kamati hizo watakaotumia fedha kinyume na miongozi iliyowekwa.

Waziri Aweso alisema hayo akizindua huduma za maji kwenye vijiji vya Migongo wilayani Buhigwe na Makere wilaya ya Kasulu alipokuwa akizindua miradi ya maji ambayo imekamilika na wananchi wameanza  kupata huduma.

Waziri huyo wa maji alisema kuwa baada ya miradi kukamilika na huduma kuanza kupatikana kwa wananchi miradi mingine inashindwa kuendelea kutoa huduma inapotokea hitilafu ndogo ya miundo kwa maelezo ya kutokuwepo kwa fedha za kufanyia matengenezo wakati wananchi wanalipa bili kwa huduma hiyo ya maji.

Alisema kuwa fedha za bili za maji zinazolipwa na wateja kazi ya kwanza ni kuzingatia kufanya matengenezo ya miundo mbinu na  kwamba hizo siyo fedha za kugawana kama sadaka na kutaka ofisi za wakuu wa wilaya, Wakurugenzi wa halmashauri na mamlaka za maji  kusimamia kwa karibu na kuchukua hatua kwa wote ambao watatumia fedha hizo kinyume cha taratibu.

Alibainisha kwamba serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji miradi  kuwezesha wananchi kupata huduma ya maji safi na salama na kwamba haikubaliki kuona miradi inasimama kutoa huduma kwa changamoto ndogo zinazojitokeza ambazo zipo kwenye uwezo wa kamati za watumia maji na fedha zipo lakini hazitumiki kutatua changamoto zinazojitokeza.

Katika hatua nyingine Waziri huyo wa maji alisema kuwa wizara yake kwa kushirikiana na wadau inatekeleza maono ya Raisi Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kwa kuhakikisha miradi mingi inatekelezwa na huduma inapatikana karibu na makazi ya watu akitaka pia kila mmoja kwa nafasi yake awe mlinzi wa miradi hiyo iweze kudumu kwa muda mrefu.

Akiwa wilayani Buhigwe Kaimu Mkuu wa wilaya hiyo,Isack Mwakisu alisema kuwa kwa sasa huduma ya maji inapatikana kwa asilimia 72 na kwamba ipo miradi mingi yenye pesa nyingi inatekelezwa ukiwemo mradi wa vijiji saba wenye thamani ya shilingi Bilioni 8.4.

Mbunge wa jimbo hilo Felix Kavejuru ameishukuru serikali ya Raisi Samia kwa kutoa fedha nyingi za miradi kwenye jimbo hilo na kwamba vijiji vyote vya jimbo hilo ambavyo havikuwa kabisa na huduma ya maji vimeshaanza utekelezaji wa miradi ya maji.

Naye Mbunge wa jimbo la Kasulu Vijijini, Augustino Hole Vuma alisema kuwa kwa mwaka wa fedha ulioisha jimbo hilo lilipatiwa kiasi cha shilingi Bilioni 6.5 ambazo zimeweza kusogeza huduma ya maji safi na salama karibu na wananchi.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI